1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya maadili kuchunguza tuhuma za ufisadi Kenya

Wakio Mbogho7 Oktoba 2022

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini Kenya imesema inazifuatilia kaunti 24 kutokana na tuhuma za kuendeleza ufisadi wa kiwango cha juu.

https://p.dw.com/p/4HtJt
Kenia | Amtseinführung Präsident William Ruto
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Tume ya EACC inafuatilia matukio ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi katika kaunti 24 kati ya kaunti 47 nchini. Ripoti iliyotolewa na Tume inayosimamia mgao wa fedha na raslimali za umma nchini Kenya imeeleza kuwa serikali za kaunti zimekuwa zikipoteza mabilioni ya pesa kila mwaka kutokana na ufisadi pamoja na mifumo isio thabiti. Mwenyekiti wa tume ya EACC Eliud Wabukhala anasema :

"Tume ya EACC inatathmini hatari ilioko kwenye vitengo mbali mbali vya serikali za kaunti. Tumefanya hivyo kwenye kaunti 24 kufikia sasa.Tumegundua changamoto hizo na tukatoa ushauri kwa mianya hiyo kuzibwa, ndiposa tuweze kuokoa pesa za umma.”,alisema Wabukhala.

Tume ya EACC vilevile ina jukumu la kuchunguza na kushauri wizara, idara na kampuni za umma.

Wakati huo huo, baraza la magavana nchini limetoa wito kuwa Rais William Ruto kuagiza hazina kuu kusambaza fedha zilizotengewa serikali za kaunti kufikia jumatatu wiki ijayo.

''Hali ilivyo sasa kwenye kaunti zote 47 nchini inahuzunisha''

Kenia wartet mit Spannung auf das Urteil des Obersten Gerichtshofs zu den Wahlen
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Mwenyekiti wa baraza hilo Anne Waiguru amesema kaunti zote nchini hazina pesa, na kwamba huduma na miradi muhimu imekwama. Waiguru ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kirinyaga, amesema serikali za kaunti zinaidai serikali ya kitaifa shilingi billion 51.7 ya miezi ya Agosti na Septemba, na wanatarajia fedha zingine shilingi bilioni 29.6 za mwezi wa Octoba.

"Hali ilivyo sasa kwenye kaunti zote 47 nchini inahuzunisha. Inasikitisha kwamba awamu ya tatu ya uongozi wa kaunti nchini inaanza bila raslimali muhimu. Tungependa kuujulisha umma kuwa, katiba ya Kenya pamoja na sera ya fedha ya mwaka 2012 imeratibu kwamba fedha zilizotengewa serikali za kaunti zinapaswa kusambazwa kwa kaunti hizo kila tarehe 15 ya mwezi bila kuchelewa.”, alisema Waiguru.

Itakumbukwa pia kwamba Rais William Ruto alipoingia mamlakani aliiondoa wizara ya ugatuzi iliyokuwa inashughulikia maswala ya kaunti. Hii inaacha pengo katika namna kaunti zinavyofadhiliwa, na baraza la magavana limetoa wito kuwa Rais Ruto kuagiza wizara ya fedha kuwezesha usambazaji wa fedha zilizotengewa serikali za kaunti.

Ushirikiano wa taasisi

Aidha, malumbano kati ya mabunge mawili, bunge la seneti na bunge la kitaifa yameifanya vigumu kutekeleza mifumo na sera inayofaa katika ukaguzi wa raslimali za kaunti. Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi aliahidi kuzika uhasama huu katika uongozi wake.

Mwenyekiti wa EACC Eliud Wabukala amehimiza ushirikiano kati ya mabunge ya serikali za kaunti na tume yao ili kufanikisha matumizi mazuri ya fedha za umma.