Tunisia yatumbukia katika mgogoro wa kikatiba
27 Julai 2021Makabiliano ya waandamanaji yalizuka jana nje ya Bunge lililowekwa chini ya ulinzi wa kijeshi, baada ya Saied kumfuta kazi Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kuamuru bunge lifungwe kwa siku 30, hatua ambayo chama kikubwa kabisa cha kisiasa nchini humo Ennahda imeeleza kuwa ni "mapinduzi" dhidi ya katiba. Lakini rais Saied ameutetea uamuzi wake."Nimechukua wajibu, ninachukua wajibu wa kihistoria. Wale wanaodai suala hili linahusiana na mapinduzi, wanahitaji kupitia upya mafunzo yao kuhusu katiba."
Soma pia: Tunisia: Rais Kais Saied amfuta kazi Waziri Mkuu Hicham Mechichi
Chama cha Ennahda ambacho ndicho mshirika mkubwa katika serikali ya muungano kimeonya kuwa wana wamachama wake watayalinda mapinduzi yaliyofanywa na umma. Mechichi amesema atakabidhi madaraka kwa mtu atakayeteuliwa na rais, katika matamshi yake ya kwanza tangu kuchukuliwa hatua hiyo ya kushangaza.
Saied alisema amechukua maamuzi yanayohitajika ili kuiokoa Tunisia, taifa, na watu wa Tunisia, kufuatia maandamano katika miji kadhaa ya kupinga namna serikali inavyolishughulikia janga la Covid.
Rais huyo, ambaye chini ya katiba analidhibiti jeshi, amewaonya wapinzani wake dhidi ya kuchukua silaha, akitishia kuwa kama yeyote atafyatua risasi moja tu, vikosi vyake vitajibu kwa mvua ya risasi. Ofisi ya rais ilitangaza jana kufutwa kazi kwa Waziri wa Ulinzi Ibrahim Bartaji na Hasna Ben Slimane, kaimu waziri wa sheria. Umoja wa Mataifa unaomba utulivu nchini humo. Farhan Haq ni naibu msemaji wa Katibu Mkuu Antonio Guterres. "Tunatumai hali itabaki kuwa tulivu, na tunajaribu kuhakikisha kuwa pande zote nchini humo zinafanya kila jitihada kuhakikisha hali inabakia tulivu. Bila shaka eneo hilo ni tete sana na hakika ni eneo ambalo halistahili tena kuwa na machafuko zaidi kama ilivyoshuhudiwa siku za nyuma." Amesema Faq.
Soma pia: Tunisia: Mvutano mkubwa baada ya rais kulisimamisha bunge
Chama Kikuu chenye ushawishi cha Wafanyakazi nchini Tunisia, UGTT ambacho kilikuwa na mchango mkubwa katika vuguvugu la umma la mwaka wa 2011, kimesema rais amefuata sheria ili kuzuia hatari inayokaribia na kurejesha utendaji wa kawaida wa taifa.
Mgogoro wa Tunisia unafuatia miezi kadhaa ya mkwamo kati ya rais, waziri mkuu na mkuu wa chama cha Ennahda Rached Channouchi ambaye ni spika wa bunge, ambao umeathiri vita dhidi ya Covid.
Uhasama huo umezuia uteuzi wa mawaziri na kupelekwa kwingine raslimali za kupambana na matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii nchini Tunisia.
Saied amesema atakamata madaraka kamili kwa msaada wa serikali ambayo itaongozwa na waziri mkuu atakayemteuwa mwenyewe. Wachambuzi wanasema haijabainika wazi kitakachofuata.
Katika kipindi cha miaka 10 tangu vuguvugu la mapinduzi lililomuondoa madarakani rais Zine El Abidine Ben Ali, Tunisia imekuwa na serikali tisa.
AFP, DPA