Tuzo ya Nobel ya uandishi fasihi
13 Oktoba 2006Kamati ya Tuzo ya Nobel nchini Sweden imemsifu mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 54 kwa kufanikiwa kutoa sura mpya ya kutetea na kuunganisha tamaduni mbali mbali.
Orhan Pamuk ni mwandishi wa kwanza wa Kituruki kutunukiwa tuzo ya Nobel ya uandishi fasihi.Vile vile ni mwandishi pekee aliekosoa hali ya sasa na historia ya Uturuki,bila ya kuogopa kueleza bayana maovu ya kale ya nchini mwake.Ukweli kuwa Orhan Pamuk hakubadili msimamo wake,licha ya kufikishwa mahakamani mara kadhaa,pamoja na kutukanwa na kukabiliwa na vitisho vya kutaka kumuua,ni sababu ya kutosha kwa Uturuki kufurahia heshima iliyotolewa kwa mtetezi wa uhuru wa mtu kueleza maoni yake.
Wakati ambapo Uturuki imepata mshtuko wa furaha kutoka chuo cha elimu ya juu cha mji wa Stockholm nchini Sweden,siku hiyo hiyo bunge la Ufaransa lilipitisha sheria inayosema,kukanusha mauaji ya Warmenia katika miaka ya 1915 na 1916 ni kosa la jinai.Habari ya kutunukiwa Pamuk,imesaidia kudhibiti hasira ya umma wa Kituruki katika midahalo mikali iliyozuka nchini humo,ikiulizwa hatua gani za kisiasa,kiuchumi na kitamaduni zichukuliwe dhidi ya Ufaransa.
Mafanikio ya uandishi fasihi wa Pamuk ni dhahiri. Kwani yeye amefanikiwa kutoa sura halisi ya mji wa Istanbul.Pamuk aliezaliwa Istanbul,ametiwa motisha na mji huo kueleza mema na maovu katika maisha ya makabila na tamaduni mbali mbali-mji ambao tangu karne kadhaa,umeshuhudia tamaduni na ustaarabu kutoka mabara matatu na vile vile umeshuhudia ufukuzaji wa watu.Pamuk,ametunukiwa kwa kufanikiwa kueleza jinsi tamaduni mbali mbali zinavyogongana na kuingiliana.
Mwaka jana alipotunukiwa zawadi ya amani ya tume ya biashara ya vitabu ya Ujerumani katika mji wa Frankfurt,Pamuk alitoa mwito wa kuanza kuiingiza nchi yake katika mfumo wa Ulaya-yaani uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya.Lakini yeye binafsi nchini Uturuki,alifikishwa mahakamani kwa sababu alizungumza juu ya “mauaji ya Warmenia milioni moja na Wakurdi 30,000” nchini mwake.Kwa kutamka hayo,kuambatana na sheria ya Kituruki, Pamuk alivunja hadhi ya Uturuki.Kesi hiyo lakini ikatupiliwa mbali na kuanzia hapo,Pamuk nchini Uturuki alikuwa msomi mbishani.Kwa upande mwingine lakini ni kwa sababu yake,sasa midahalo ya hadhara kuhusu suala la Warmenia imevunja miko na uhuru wa mtu kutoa maoni yake umenawiri upya.
Labda tuzo ya Nobel ya uandishi fasihi alietunukiwa Pamuk itasaidia majadiliano yasio rasmi kati ya Waturuki na Warmenia juu ya njia ya kukabiliana na historia yao na kusawazisha uhusiano wa ujirani.Litakuwa jambo la busara kama serikali ya Ankara itajipatia nguvu mpya kutokana na tuzo hii,badala ya kugubikwa na hasira yake kuhusu sheria iliyoidhinishwa na Ufaransa.