UAE yamteua bosi wa shirika la mafuta kuongoza COP28
12 Januari 2023Mamlaka za Abu Dhabi zimemteua Sultan Ahmed al-Jaber, ambaye ni mshirika wa kuaminika wa kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, kuongoza mkutano wa kimataifa wa mazingira kwa mwaka huu wa COP28.
Soma: Mkutano wa COP27 waanza kwa onyo Misri
Taarifa iliyotolewa na shirika la habari la nchi hiyo WAM imesema kwamba Sultan al-Jaber anakuwa mkurugenzi wa kwanza kuchukua jukumu katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa. WAM imemnukuu al-Jaber akisema kuwa "huu utakuwa mwaka muhimu katika muongo muhimu kwa hatua za mabadiliko ya tabia nchi. Umoja wa Falme za Kiarabu unaelekea COP28 ikiwa na ari ya uwajibikaji''
Taarifa hiyo imeongeza kuwa nchi hiyo imewekeza "zaidi ya dola bilioni 50 za Kimarekani katika miradi ya nishati mbadala kwenye nchi zipatazo 70, ikiwa na mipango ya kuwekeza wastani wa dola zingine bilioni 50 katika muongo ujao". Hata hivyo uteuzi wake umeibua ukosoaji wa haraka kutoka kwa wanaharakati wa mazingira wakionya kwamba ushirikishwaji wa mtu mkubwa kutoka sekta ya mafuta kunaweza kudhoofisha hatua za mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani.
Umoja wa Falme za Kiarabu, moja ya mzalishaji mkubwa wa mafuta ghafi dunia, inadai kwamba mafuta yanasalia kuwa na umuhimu mkubwa katika uchumi wa dunia. "Umoja wa Falme za Kiarabu imejitolea kwa ushirikiano wa kimataifa na mchakato shirikishi unaoleta pamoja uchumi unaochipukia na mataifa yaliyoendelea, mashirika ya kiraia, na biashara ili kufikia suluhisho na kasi ya mabadiliko inayohitajika," ilisema taarifa hiyo.
Nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mazingira wa COP28 utakaofanyika mjini Dubai kati ya mwezi Novemba na Desemba. Mkutano uliopita wa COP27 uliofanyika nchini Misri mwaka uliopita, ulikamilika kwa wajumbe kukubaliana juu ya azimio la kuyasaidia mataifa maskini yaliyoathirika na mabadiliko ya tabia nchi lakini ulishindwa kuweka malengo mapya juu ya kupunguzwa kwa uzalishaji wa gesi chafu.
Umoja wa Falme za Kiarabu ni mojawapo ya nchi zilizo katika hatari kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi kutokana na kwamba iko katika moja ya maeneo yenye joto kali zaidi duniani, huku joto wakati wa kiangazi ikipindukia nyuzi joto 50. Kulingana na utafiti uliochapishwa mnamo mwaka 2021, sehemu za Ghuba zinaweza kuwa na joto kali kwa makaazi ya wanadamu kufikia mwisho wa karne hii.