Ubalozi wa Israel nchini Misri, washambuliwa
10 Septemba 2011Balozi wa Israel nchini Misri ameripotiwa kuondoka nchini humo mapema leo, kurejea nyumbani.
Rais Barack Obama wa Marekani ameitaka Misri kuulinda ubalozi huo dhidi ya waandamanaji na katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameeleza wasiwasi wake kuhusu tukio hilo.
Mamia ya polisi na wanajeshi wamepambana na waandamanaji ambao jana usiku, waliuvunja uzio unaozunguka jengo la ubalozi wa Israel mjini Cairo. Uzio huo ulijengwa na serikali ya Misri baada ya maandamano kufanywa kila siku nje ya ubalozi wa Israel, kupinga mauaji ya walinzi watano wa mpakani wa Misri, katika mji wa Sinai.
Walinzi hao waliuawa kwenye mpaka wa Misri, katika shambulio la Israel lililowalenga wapiganaji wa Kipalestina.
Kufuatia ghasia hizo za waandamanaji mjini Cairo, Misri imetangaza tahadhari ya hali ya juu.