Makadirio yaonesha mchuano mkali kati ya CDU/CSU na SPD
26 Septemba 2021Chama cha mrengo wa wastani wa kushoto cha Ujerumani SPD kulikuwa katika mchuano mkali na muungano wa kansela anaeondoka Angela Merkel katika uchaguzi wa bunge, katika kura ambayo itaamua nani anarithi mikoba ya kiongozi huyo wa muda mrefu baada ya miaka 16 madarakani, kwa mujibu wa makadirio ya matokeo ya awali. Maafisa kutoka vyama vyote wamesema wanatumai kuongoza serikali ijayo.
Makadirio ya awali yaliotolewa na kituo cha utangazaji wa umma yanaonesha uungaji mkono wa asilimia 25 kwa kila chama kwa chama cha Social Democratic SPD, ambacho naibu kansela anaemaliza muda wake na waziri wa fedha Olaf Scholz, anawania nafasi ya kansela - na muungano wa kati-kulia wa Merkel chini ya Armin Laschet.
Makadirio mengine ya sirika la utangazaji la umma la ZDF yamekiweka chama cha SPD mbele kwa asilimia 26 dhidi ya 24. Makadirio hayo yamekiweka chama cha watetezi wa mazingira, die Grüne, katika nafasi ya tatu kwa ailimia 15.
Kwa kuzingatia makadirio hayo, kuunda serikali ijayo ya muungano katika taifa hilo kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya kunaweza kuwa mchakato mrefu na mgumu. Merkel atabakia kuwa kiongozi wa muda hadi serikali mpya itakapoundwa.
Makadirio hayo ya matokeo yamekipa chama cha kiliberali cha FDP asilimia 11-12 na chama cha mrengo wa kushoto asilimia 5. Chama cha mrengo mkali wa kulia AfD kinaonekana kupata asilimia 11 ya kura.