Uchaguzi wa Ghana 2020 ni kushindwa kwa Demokrasia
10 Desemba 2020
Rais Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic Party NPP, ameibuka mshindi baada ya kujizolea asilimia 51.59 ya kura zilizopigwa. Uchaguzi huo unachukuliwa kama ushindi kwa Ghana. Hiyo ni kwa sababu, nchi hiyo kwa mara nyingine, imefanikiwa kuendesha uchaguzi wa amani bila ya kuchomwa nyumba na kuvunja viungo na mafuvu ya vichwa vya watu ambavyo mara nyingi huonesha namna uchaguzi wa Afrika ulivyo.
Au, kuwa sahihi zaidi, inamaanisha kwamba vifo na uharibifu uliotokea Ghana havikuwa na maana ukilinganisha na nchi zingine barani Afrika. Kwa hayo, Ghana imeendelea kushikilia nafasi ya kinara wa demokrasia Afrika. Lakini sifa hiyo inazidi kutia mashaka wakati Ghana ikikabiliwa na mtihani wa utawala bora na demokrasia ya kweli.
Chaguzi za amani ziwe tamaduni
Wakati Wajerumani wanapopiga kura, hatusikii hofu ya kutokea vurugu. Vivyo hivyo kwa Wafaransa na nchi nyingine za Ulaya, ambako kunakuwa na makabidhiano ya amani ya madaraka. Hata wakati rais wa Marekani Donald Trump alipotusaidia kutambua ubaya wa siasa na uchaguzi wa Marekani, bado hatukuona vurugu, vifo, ubakaji na mateso. Swali ni je kwa nini uchaguzi wa amani uchukuliwe tu kuwa mafanikio ya kipekee barani Afrika?
Ninaamini kile kinachotokea kati ya uchaguzi wa amani ndicho chenye kutia mashaka. Kwa Mghana wa kawaida, hakuna namna ya kuwawajibisha waliochaguliwa mbali na kusubiri hadi miaka minne ijayo kufanya hivyo kupitia uchaguzi. Sababu ni moja tu kwamba uchaguzi umeshindwa kuwa nyenzo ya uwajibikaji katika nchi ambayo pande zote mbili za kisiasa zinazosimamia hatma ya Ghana zimeonekana kufanya kazi na kauli mbiu moja ya "kuwa na msemo wako na niruhusu niwe na njia yangu”.
Vyama vya NDC na NPP ni kama pande mbili za sarafu. Ni mapacha wanaofanana ambao hutofautishwa tu kwa majina, na kwamba huwa wanajali tu pindi wanapokuwa upande wa upinzani.
Tatizo la siasa za Ghana zinatokana na mfumo wake wa madaraka.
Matokeo ya uchaguzi wa 2020 yanamaanisha vyama vya NDC na NPP kila kimoja kimeshinda uchaguzi mara nne tangu mwaka 1992 wakati Ghana iliporejea katika mfumo wa vyama vingi. Sio tu vyama vile vile ambavyo vimesalia kuwa madarakani, lakini pia ni mara ya tatu ambapo John Mahama na Akufo-Addo wanashindana katika uchaguzi wa urais.
Demokrasia imeshindwa kuimarika Ghana
Kwa mtizamo wa viashiria vya utawala bora, tungesema hata kama demokrasia inakua Ghana lakini haikomai. Kwa njia tofauti demokrasia inazidi kuwa mbaya. Polisi hadi hivi sasa wameshindwa kuwapata waliohusika katika mauaji ya mwandishi wa habari za uchunguzi Ahmed Hussein-Suale, ambaye alitishiwa na mwanasiasa wa chama cha rais Akufo-Addo mwaka jana. Nchi pia imeshindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha kukamatwa, kufungwa na madai ya kuteswa kwa waandishi wa habari wa tovuti ya Modern Ghana.
Hakuna matumaini makubwa ya Ghana kati ya sasa na uchaguzi ujao wa 2024. Hiyo ni kwa sababu, kama ilivyo kwa mataifa mengi ya Afrika, ufisadi na upotevu ni changamoto katika maendeleo ya Ghana. Rais Akufo-Addo alipata ushindi wa kushawishi mwaka 2016, kwa sababu tu serikali ya Mahama ilikuwa ikishutumiwa vikali na ufisadi.
Serikali ya Akufo-Addo nayo pia imekumbwa na kashfa hizo hizo za ufisadi. Kiuhalisia, rushwa ndio imesababisha chama chake kutikisika katika uchaguzi wa mwaka huu licha ya kufuta ada za shule kwa sekondari, upatikanaji wa maji bure na umeme mwaka 2020 pamoja na utekelezaji wa miradi mingi.
Kinachofanya hali ya sasa kuwa mbaya zaidi au kukosa matumani kabisa ni taasisi za uwajibikaji ambazo zinalengwa na kudhoofishwa. Serikali ya Akufo-Addo inatajwa kukopa pesa nyingi katika muhula wake wa kwanza kuliko walivyokopa marais wote tangu nchi ipate uhuru. Shirika la fedha ulimwenguni linakadiria kuwa deni la Ghana kwa uwiano wa pato la taifa lifafikia asilimia 74.7 hapo mwakani. Wakati kodi na vyanzo vingine vya fedha vikiendelea kuvuja, nchi inakabiliwa na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na matumizi yasiyo ya lazima katika uchaguzi wa mwaka huu na janga la virusi vya corona.