1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mchujo wafanyika New York

Admin.WagnerD19 Aprili 2016

Wapigaji kura wa jimbo la New York wanapiga kura leo (19.04.2016) katika chaguzi za awali kumtafuta mgombea urais wa vyama vya Democtratic na Republican. Clinton na Trump wanatarajiwa kushinda.

https://p.dw.com/p/1IYbu
US Vorwahlen New York Hillary and Bill Clinton
Hillary Clinton, kushoto, na mumewe, Bill ClintonPicha: Reuters/M. Segar

Mgombea wa chama cha Republican anayetafuta uteuzi wa kuwania urais wa Marekani katika uchaguzi ujao Novemba mwaka huu, Donald Trump na mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton, wana matumaini mafungamano waliyo nayo kwa wakazi wa jimbo la New Yok yatawasaidia kuimarisha ushindi wao, huku wapigaji kura katika jimbo hilo wakipiga kura leo katika uchaguzi wa mchujo.

Upigaji kura umeanza katika jimbo la New York unaotarajiwa kumpa ushindi Hillary Clinton na Donald Trump, katika kinyang'anyiro cha kuwania tiketi ya kuelekea ikulu.

Clinton, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje aliyewahi kuchaguliwa mara mbili kama seneta wa jimbo la New York, anaongoza kura za maoni dhidi ya mpinzani wake seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders, licha ya kwamba kura za maoni kitaifa zinawaonyesha wagombea hao wakikabana koo. Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na vinatarajiwa kufungwa saa tatu usiku.

Muda mfupi baada ya kupiga kura na mumewe, rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Hillary Clinton alisema, "Nina furaha kuhusu kufanya kampeni na kupiga kura hapa New York. Naipenda New York na natumai kila mtu atajitokeza kupiga kura. Ninamhimiza kila mtu, tafadhali jitokeze upige kura kabla saa tatu usiku leo. Hilo litakuwa jambo la maana sana. Asanteni sana."

Kombobild Donald Trump, Ted Cruz, John Kasich
Picha: picture-alliance/AP Photo

Sanders hana bahati New York kwa kuwa wanachama milioni 5.8 wa chama cha Democratic na Warepublican milioni 2.7 wamejiandikisha kupiga kura. Watu wengine wasio wanachama wa vyama hivi vya siasa hawaruhusiwi kupiga kura.

Clinton aelekea kushinda uteuzi

Clinton ameungwa mkono na wajumbe 1,790 ikilinganishwa na Sanders akiwa na wajumbe 1.113, na hivyo yuko katika nafasi nzuri ya kufikisha idadi ya wajumbe 2,383 inayohitajika kushinda uteuzi wa chama kugombea urais wa Marekani.

Wagombea watatu wanaliona jimbo la New York kuwa nyumbani: Clinton aliwahi kuwa seneta wa New York mara mbili na Sanders alilelewa Brooklyn, New York. Trump alizaliwa Queens mjini New York, na hajawahi kuishi mahala pengine na hivi sasa anaishi katika jengo lenye jina lake mjini Manhattan.

Akiuhutubia mkutano wa hadhara katika taasisi ya Niagara, huko Buffalo, New York, Trump alisema, "Ningependa kuzungumzia maadili ya New York ambayo sote tunayafhamu vizuri sana. Maadili yanayotuifanya tulipende jimbo hili licha ya mataizo yake. Tulipenda jimbo hili. Tunafahamu litainuka tena. Nikiwa rais litainuka haraka sana hamtaamini."

Kura za maoni zinaonyesha Trump anatarajiwa kuwashinda wapinzani wake wote, seneta wa jimbo la Texas, Ted Cruz na gavana wa Ohio, John Kasich. Trump anaungwa mkono na asilimia karibu 50 ya wajumbe huku Cruz na Kasich wakiungwa mkono na asilimia takriban 20 ya wajumbe kila mmoja.

Mwandishi:Josephat Charo/ape/reuters

Mhariri:Yusuf Saumu