Uchaguzi wa Ujerumani: Kwanini Elon Musk anaipigia debe AfD?
1 Januari 2025Bilionea wa teknolojia wa Marekani, Elon Musk, siku ya Jumamosi alisisitiza tena kukiunga mkono chama cha mrengo mkali wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD) kupitia makala ya maoni iliyochapishwa na gazeti la Welt am Sonntag.
Hii ilijiri siku chache baada ya Musk kuandika kwenye mtandao wake wa kijamii, X, kwamba "ni AfD pekee inayoweza kuiokoa Ujerumani."
Aliandika kuwa chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia kilikuwa "cheche ya mwisho ya matumaini kwa nchi," akidai kuwa Ujerumani iko ukingoni mwa "kuporomoka kiuchumi na kitamaduni," na kwamba ni chama hicho pekee kinachoweza kufufua uchumi wa Ujerumani na kuzuia kupoteza utambulisho wake kupitia "sera ya uhamiaji usiyodhibitiwa."
Soma pia: Kansela Scholz: 'Tunaweza kufanya 2025 kuwa mwaka mzuri'
"Kwa wale wanaoikosoa AfD kama chama cha misimamo mikali, nawaambia: msiruhusu sifa hiyo iwavunje moyo," Musk aliandika. "Kuionyesha AfD kama chama cha msimamo mkali wa kulia si sahihi, ukizingatia kwamba Alice Weidel, kiongozi wa chama hicho, ana mpenzi wa jinsia moja kutoka Sri Lanka! Je, hiyo inasikika kama Hitler kwenu? Tafadhali!"
Katika makala hiyo iliyochapishwa kwa Kijerumani, Musk pia aliisifu njia ya AfD kuhusu kanuni, kodi, na kuondoa vizuizi vya soko.
Ingawa makala hiyo ilichapishwa kama makala ya maoni na mhariri mkuu mteule wa Welt, Jan Philipp Burgard, uamuzi wa kuichapisha ulikabiliwa na upinzani kutoka kwa wahariri wa Welt na kusababisha kujiuzulu kwa mhariri mwandamizi wa tolea la Jumapili la gazeti hilo la Welt am Sonntag.
Wimbi la hasira
Friedrich Merz, mgombea wa ukansela wa muungano wa byama vya mrengo wa kati wa kulia katika uchaguzi wa bunge utakaofanyika Februari 23, alikosoa vikali makala ya Musk, akiiita "uingiliaji wa dharau."
AfD kwa sasa ina asilimia 20 katika kura za maoni, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya muungano wa kihafidhina wa Christian Democratic Union (CDU) na Christian Social Union (CSU) unaoongozwa na Merz.
Mwenyekiti wa chama cha mrengo wa kati wa kushoto cha Social Democrats (SPD), Lars Klingbeil, alimshtumu Musk kwa kutaka "kuizamisha Ujerumani katika machafuko" na kumfananisha na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
"Wote wawili wanataka kuathiri uchaguzi wetu na hasa kuunga mkono maadui wa demokrasia, AfD," Klingbeil alisema.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari cha DJV, Mika Beuster, alizionya ofisi za uhariri zisiruhusu zenyewe kutumiwa kama vyombo vya propaganda wakati wa maandalizi ya uchaguzi mkuu, lakini zichukue tahadhari kubwa zinaposhughulikia makala za wageni.
"Vyombo vya habari vya Ujerumani havipaswi kujiruhusu kutumiwa kama vipaza sauti vya watawala wa kimabavu na marafiki zao," alisema.
Uhuru wa vyombo vya habari au kampeni ya uchaguzi?
Je, vyombo vya habari nchini Ujerumani vinaweza kuunga mkono au kupinga wagombea wa kisiasa wakati wa kampeni za uchaguzi? Jibu ni ndiyo, inaruhusiwa nchini Ujerumani, lakini ni jambo la nadra kufanyika. Uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari vimewekwa wazi katika katiba.
Soma pia: Chapisho la Musk kuhusu AfD lawakera wanasiasa wa Ujerumani na kujibiwa kwa ghadhabu
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Msingi ya Ujerumani kinasema: "Kila mtu atakuwa na haki ya kujieleza na kusambaza maoni yake kwa uhuru kwa maneno, maandishi na picha na kupata habari bila kizuizi kutoka kwa vyanzo vinavyopatikana kwa ujumla.
Uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kuripoti kwa njia ya matangazo na filamu utahakikishwa. Hakutakuwa na udhibiti. Haki hizi zitakuwa na mipaka kwa mujibu wa sheria za jumla, masharti ya ulinzi wa vijana, na haki ya heshima ya mtu binafsi."
Mwaka wa 2002 kwa mara ya kwanza, gazeti la Financial Times Deutschland liliunga mkono chama fulani katika uchaguzi wa Ujerumani: Lilitenga ukurasa mzima ulioelezwa kuwa maoni kuwashawishi wasomaji kuipigia kura CDU, na kuongeza ukurasa wa pili kuelezea walivyofikia uamuzi huo.
Uhusiano kati ya Musk na Welt
Haijulikani wazi jinsi makala ya Musk ilivyolifikia gazeti la kihafidhina Welt, ambalo linamilikiwa na kundi la Springer. Mathias Döpfner, Mkurugenzi Mtendaji wa Springer, amewahi kuonyesha kuvutiwa na Musk hapo awali, na inasemekana wana mawasiliano ya kibinafsi.
Döpfner mara kadhaa amezua mjadala pale jumbe zake za ndani na barua pepe alizotuma kwa washirika wake zilipoanikwa hadharani, zikionyesha akikosoa hatua za kupambana na janga la COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi.
Soma pia: Wajerumani wakasirishwa na Musk kuinga mkono AfD
Pia alijaribu kushawishi ripoti za gazeti la Bild ziunge mkono chama cha Free Democrats (FDP) kabla ya uchaguzi wa shirikisho wa 2021. Alisema: "Tumaini letu la mwisho ni FDP," na kwamba ushindi wa chama hicho kingezuia "janga la nyekundu-kijani," Döpfner aliripotiwa kuandika, akionya juu ya serikali ya muungano ya vyama vya SPD na KIjani.
Malengo ya Musk
Tajiri huyo mkubwa zaidi duniani, kimsingi, anaonekana kuwa na maslahi yake ya kiuchumi akilini. Katika makala yake, Musk aliisifu AfD kwa mipango yake ya "kupunguza kanuni za serikali, kupunguza kodi, na kuondoa vizuizi vya soko."
Kiwanda cha Tesla kilicho Brandenburg, nje ya Berlin, ambacho ni kiwanda cha kwanza cha magari ya umeme cha mtengenezaji huyo wa Marekani barani Ulaya, kingeweza kufaidika na mabadiliko hayo.
Hata hivyo, Musk, mwenye wafuasi milioni 200 mtandaoni duniani kote, anaonekana kuendesha ajenda ya kisiasa ya kimataifa ya kukuza nguvu za mrengo wa kulia. Inasemekana aliwaahidi wapinga mfumo wa kisiasa wa Uingereza wa chama cha Nigel Farage mchango wa €95 milioni.
Nchini Ujerumani, msaada wa Musk kwa AfD unaweza kufungua milango kwa vikundi vya mrengo wa kulia kuongeza mwonekano wao na kuhalalisha simulizi zao.