Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wahitimisha kampeni
25 Septemba 2021Utafiti wa maoni ya raia unaonesha tofauti ndogo kati ya wagombea hao huku Scholz wa chama kinachofuata nadharia ya mrengo wa wastani wa kushoto SPD akiwa mbele ya Laschet wa CDU kwa asilimia tatu pekee.
Kansela anayemaliza muda wake Angela Merkel, ambaye ameliongoza taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya kwa karibu miaka 16, anamuunga mkono mwanachama mwenzake wa chama cha kihafidhina cha CDU Armin Laschet, katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni huko Aachen alikozaliwa mgombea huyo.
Scholz wa chama cha SPD yuko kwenye kampeni za mwisho katika jimbo la Brandenburg, lililo karibu na mji mkuu. Mgombea wa tatu kutoka chama cha kijani, Annalena Baerbock, amehitimisha kampeni zake akiwa kwenye nafasi ya tatu katika utafiti huo wa maoni, huku akipewa nafasi ndogo ya kuwa kansela. Hata hivyo chama chake kinatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi yake kwenye uchaguzi huu ikilinganishwa na ule wa mwaka 2017, na huenda kikahusika katika kuunda serikali ya pamoja.
Muungano wa vyama vitatu unatarajiwa
Waangalizi wengi wa uchaguzi wanatarajia matokeo yatasababisha kuwa na serikali inayohusisha vyama vitatu, lakini bado haijawa wazi ni vyama vipi vitakavyokuwemo. Ikiwa kambi ya Laschet inayoundwa na vyama ndugu CDU/CSU kitaongoza, serikali ya muungano itakayoundwa inatarajiwa kuwa ya mrengo wa kati na kulia.
Kama chama cha SPD kikishinda, basi Ujerumani inaweza ikabadilika kidogo ama kuchukua kabisa mwelekeo mpya wa siasa za mrengo wa kushoto kutegemeana na ni nani atakayechaguliwa na Scholz kuwa mshirika wake. Uwezekano mwingine ni kuwa Ujerumani inaweza kuendelea na serikali ya muungano wake wa sasa unaoundwa na vyama vya SPD na CDU/CSU