Trump na Harris wakabana koo kuelekea White House
9 Septemba 2024Utafiti huu unatolewa wakati ambapo washindani hao wanatarajiwa kupambana kwa hoja kwenye mdahalo utakaoonyeshwa kwenye televisheni kwa mara ya kwanza.
Utafiti wa hivi karibuni unathibitisha kwamba Trump anaendelea kuungwa mkono na takriban nusu ya wapiga kura, licha ya sifa mbaya kama mhalifu aliyehukumiwa, na licha ya dhima yake katika kujaribu kuyabadilisha mateko ya uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo Rais Joe Biden alishinda.
Hata hivyo, utafiti unaonesha kwamba Harris, bado hajapiga hatua kubwa mbele. Matokeo ya utafiti wa maoni ya wapigakura uliofanywa kwa ushirikiano wa New York Times na taasisi ya utafiti ya Siena yameonesha kuwa katika nchi nzima Trump yupo mbele kwa asilimia 48 wakati Harris ana asilimia 47.
Utafiti huo wa maoni umeonesha kuwa Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 59, anaongoza katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania, na wagombea wa urais wako sambamba katika majimbo mengine manne ya Nevada, Georgia, North Carolina na Arizona.