Udukuzi watishia biashara ya mabilioni
31 Oktoba 2013Idadi inayoongezeka ya maafisa wa Ulaya wanatowa wito wa kusitishwa kwa makubaliano yanayojulikana kama ya "eneo salama" ambayo yanaruhusu makampuni ya Marekani kufanya mauzo ya data za kibiashara na kibinafsi, baruwa pepe na picha kutoka kwa wateja barani Ulaya. Makubaliano hayo ambayo hayajulikani sana lakini muhimu yanayaruhusu makampuni ya Marekani zaidi ya 4,200 kufanya biashara barani Ulaya yakiwemo makampuni makubwa ya mtandao kama vile Apple, Google, Facebook na Amazon.
Kufichuka kwa kiwango cha upelelezi unaofanywa na Marekani kwa washirika wake wa Ulaya pia kunatishia kutibua mojawapo ya malengo makuu ya Rais Barack Obama wa Marekani kwa uhusiano kati ya Marekani na Ulaya: makubaliano makubwa ya kibiashara ambayo yataongezea dola bilioni 138 sawa na euro bilioni 100 kwa mwaka kwa pato la uchumi ndani ya nchi kwa pande zote mbili.
Uaminifu umevunjika
Maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya wanasema uaminifu uliokuwa ukihitajika kwa ajili ya mazungumzo hayo umevunjwa.
Kamishna wa Haki wa Umoja wa Ulaya, Viviane Reding, amesema katika hotuba yake kwenye Chuo Kikuu cha Yale hapo jana kwamba ili mazungumzo magumu na makubwa yaweze kufanikiwa inabidi kuwepo uaminifu miongoni mwa washirika wa mazungumzo.
Maafisa wa Ulaya wanatarajiwa kudai Marekani iimarishe kwa kiasi kikubwa sheria zake za masuala ya faragha ili kuwapa wateja wake udhibiti zaidi juu ya namna kampuni zitakavyopaswa kutumia data zao binafsi na kuzitanuwa haki hizo kuweza kuwafikia raia wa Ulaya na hata kuwapa haki ya kuzishtaki kampuni za Marekani katika mahakama za Marekani.
Ulaya imekuwa ikishinikiza madai hayo kwa muda mrefu lakini tokea mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani, NSA, Edward Snowden, alipoanza kufichuwa habari za kushangaza za upelelezi unaofanywa na Marekani barani Ulaya, madai yao yamezidi kupata hoja.
Google na Yahoo zadukizwa
Kashfa ya upelelezi wa shirika hilo la usalama wa taifa la Marekani, NSA, inazidi kutapakaa baada ya kubainika kwamba imekuwa ikidukiza mawasiliano makuu yenye kuunganisha vituo vya data vya kampuni za mitandao za Yahoo na Google duniani kote.
Gazeti la Washington Post limeripoti hapo jana kwamba taarifa za siri za tarehe 9 Januari mwaka 2013 zimedokeza kwamba NSA imekuwa ikituma rekodi za mamilioni ya mawasiliano kila siku kutoka mitandao ya ndani ya Yahoo na Google kwenda kwenye ghala ya data katika makao makuu ya shirika hilo yaliyoko Fort Meade, Maryland mjini Washington, Marekani.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Washington Post katika kipindi cha siku 30 zilizopita wakusanyaji wa data wameshughulikia na kutuma zaidi ya rekodi mpya za mawasiliano 180 milioni kuanzia za "metadata" ambazo zingelidokeza nani aliyetuma baruwa pepe na wakati gani na maudhui yake yawe katika maandishi, sauti na video.
Kufichuliwa kwa taarifa hizo kumepokelewa kwa ghadhabu na kampuni ya Google na kuzusha masuala ya kisheria ikiwa ni pamoja na iwapo shirika hilo la NSA yumkini likawa linakiuka sheria za nchi taifa kuhusu udukuzi wa mawasiliano.
Mwandishi:Mohamed Dahman/AP
Mhariri:Josephat Charo