Uendeshaji bandari ya Zanzibar rasmi mikononi mwa muwekezaji
19 Septemba 2023Wafanyakazi kadhaa, wengi wao wakiwa wachukuzi wa mizigo na wanaoingiza vyakula kutoka Tanzania Bara walilalamikia kile walichosema ni "mabadiliko ya ghafla bila ya kupewa muda wa kujitayarisha" juu ya utaratibu wa kuingiza na kutowa mizigo, ikiwemo amri ya kuvaa sare mpya na kuwa vitambulisho rasmi.
Mmoja wa wafanyakazi hao aliiambia DW kwamba kwa sasa hawajuwi hatima yao. "Tunazunguka tu, mpaka sasa hatujapata maelezo tunayoweza kusema yamenyooka!” aliongeza.
Omar Makame, ambaye ni wakala wa uingizaji wa mizigo bandarini alisema kwamba kabla ya kuanza kazi wa kampuni ya AGL, walikuwa wakilipia shilingi 77,000 kwa kontena la tani sita, lakini sasa hivi wanalipia shilingi 200,000.
Soma: Upinzani wanusa harufu ya ufisadi Zanzibar
"Serikali inahitaji kutuangalia zaidi katika hali duni tulizonazo. Tunahitaji kusaidiwa kwani tutashindwa kujiendesha katika maisha kwa kuwa tunategemea kipato chetu kinatokane na bandari." Alisema.
Wafanyabiashara wengine waliozungumza na DW walisema kwao wao sio tu suala la kupandishwa kwa gharama bali pia kutokupewa taarifa ya uamuzi huo mapema, jambo lililosababisha bidhaa za matunda, mbogamboga na nafaka walizoingiza kutoka Tanzania Bara kuanza kuharibika.
"Sisi bidhaa zetu ni mbogamboga kama tungule, mbatata, vitunguu na karoti. Bidhaa hizi huwa hazikai kabisa. Zikizidi siku moja zinaharibika. Na tumeleta jana mpaka leo hii hatujazipata bidhaa zetu. Hivyo ni hasara na sisi hali zetu duni tunajitaji msaada wa serikali na isitizame wale wawekezaji tu. Sisi wananchi tuna haki pia” alisema Sharif Hassan ambaye anafanya kazi katika bandari ya Malindi.
Serikali kupata asilimia 30 ya faida
Shirika la Bandari la Zanzibar chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Nahaat Mohamed Mahfoudh, lilifikia makubaliano ya kukabidhisha usimamizi na uendeshaji wa bandari kuu ya Malindi kwa kampuni ya AGL kutoka Ufaransa kwa muda wa miaka mitano.
Katika makubaliano hayo, serikali ya Zanzibar itapata asilimia 30 na kampuni ya AGL kutoka Ufaransa itapata asilimia 70 ya mapato yatakayokusanywa katika bandari hiyo.
Kwenye makabidhiano rasmi, Mahfoudh alielezea matumaini yake kuwa mabakidhiano hayo kuwa yangelileta ufanisi mkubwa wa kazi katika upakuaji na uteremshaji wa mizigo bandarini hapo na kuondosha changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa mizigo.
"Kukabidhi usimamizi wa bandari ni kwa sababu ya kuleta ufanisi katika utendaji na uendeshaji wa bandari, kuongeza zana ili kuendesha inavyotakiwa na kuongeza tija na uwezo wa kuiendesha bandari kwa ujumla," alisema mkurugenzi huyo.
Mafoudh alisema miongoni mwa marekebisho yaliyokubaliwa kutekelezwa ni kuweka mikakati na kuifanya bandari iwe inakwenda katika mifumo ya kisasa na "upangaji wa makontena, kujenga bandari kavu na kujaribu kubadilisha tabia na utamaduni ambao umezoeleka bandarini."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Bandari, Joseph Meza, alisema kampuni ya AGL "itashughulika kuendesha bandari ya Malindi katika ushushaji wa mizigo tu," lakini masuala ya usafirishaji wa abiria na umiliki na bandari nyengine tano yatashughulikiwa na lenyewe Shirika la Bandari.
"Shughuli za bandari zina changamoto nyingi na hivyo serikali imeamuwa sekta binafsi na sekta za umma zifanye kazi kwa pamoja kama ambavyo serikali nyingi duniani huwa zinatumia mfumo huo wa mashirikiano, lengo likiwa ni kuzidisha ufanisi wa kazi." Alisema mwenyekiti huyo wa shirika la bandari.
Imetayarishwa na Salma Said/DW Zanzibar