Ufaransa, England zapigiwa upatu kubeba Euro 2024
6 Juni 2024Hata hivyo, timu tatu ndio zinazopigiwa upatu kutawazwa masogora wa kandanda barani Ulaya nazo ni Ufaransa, Uingereza na wenyeji Ujerumani.
Maandalizi ya mashindano haya ya mwezi mzima ni muhimu ukizingatia jinsi mashindano yaliyofanyika miaka mitatu iliyopita yalivyokuwa, kimya kimya kutokana na janga la Uviko-19 na yalichezwa kote barani Ulaya badala ya kuandaliwa na taifa moja na idadi ndogo ya mashabiki ndio waliokubaliwa kuingia uwanjani.
Soma pia: Toni Kroos kutundika daluga baada ya EURO 2024
Wakati huu mashabiki wote watashuka katika viwanja kumi vya Ujerumani, wengi wakiwa na kumbukumbu za mwaka usiosahaulika wa 2006 ambao ndio ulikuwa wa mwisho Ujerumani kuwa mwandalizi wa mashindano makuu.
Katika mashindano ya mwaka 2006, Ujerumani ilifika hatua ya nusu fainali licha ya maswali kuibuka kabla kuanza kwa mashindano yenyewe kuhusiana na uwezo wa timu ya taifa ya Die Mannshcaft.
Safari hii, kuna gumzo sawia na hilo ukizingatia kwamba Ujerumani imeondolewa kutoka kwenye mashindano mawili yaliyopita ya Kombe la Dunia mara mbili katika hatua ya makundi na mashindano ya Euro yaliyopita waliyaaga mashindano hayo katika hatua ya mtoano ya 16 bora.
Soma pia: EURO 2024: Kikosi cha Uholanzi
Lakini utakuwa ujuha kusema kwamba Ujerumani hawana nafasi ya kulishinda kombe hilo mwaka huu ukizingatia wacheza walio nao. Kocha wao Julian Nagelsmann anasema anahisi kwamba wanaweza kulishinda taji hilo.
Ila kuna Ufaransa na England, timu mbili ambazo zinapigiwa upatu na wengi kuwa zinaweza kuibuka na ubingwa. Ufaransa ndiyo timu ya Ulaya inayoorodheshwa juu zaidi katika orodha ya shirikisho la kandanda duniani FIFA ya timu bora na imetinga fainali mbili zilizopita za Kombe la Dunia, ikishinda fainali moja na kupoteza moja.
Timu hiii ina hamu sana ya kushinda taji lao la kwanza la Ulaya tangu mwaka 2000 walipokuwa wachezaji kama kina Zinedine Zidane na Thierry Henry. Safari hii lakini mbali na nyota wao Kylian Mbappe, kuna wachezaji wengi kwenye kikosi chao walio na uzoefu na ubora wa hali ya juu.
England kwa upande wao, wanaingia kwenye mashindano hayo wakifahamu kwamba hawajayashinda kwani mashindano yaliyopita mwaka 2021 waliipoteza fainali kwa mikwaju ya penalti mikononi mwa Italia. Na katika Kombe la Dunia lililopita huko Qatar, walifungwa na Ufaransa katika robo fainali.
Lakini katika mashindano haya, wana wachezaji ambao wanaweza kuwategemea pakubwa, Harry Kane na Jude Bellingham. Wote hawa wanaifahamu Ujerumani vyema, Kane akiwa ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga na Bellingham ambaye kwa sasa yuko Real Madrid, aliwahi kucheza katika klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund.