1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaionya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya 2015

Sylvia Mwehozi
17 Februari 2022

Ufaransa imeionya Iran kuwa imebakiwa na muda kidogo wa kuafikiana juu ya mpango wake wa nyuklia katika mazungumzo ya Vienna huku mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo akisema makubaliano yako karibu kufikiwa. 

https://p.dw.com/p/478tY
Österreich | Atomgespräche mit dem Iran
Picha: Joe Klamar/AFP

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alilieleza bunge siku ya Jumatano, kwamba mazungumzo ya kuokoa makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu duniani, yamefikia hatua ya mwisho na yanaweza kukamilika ndani ya siku chache zijazo. "Sio suala la wiki, ni suala la siku tu", alisema waziri Le Drian akiongeza kuwa mgogoro mkubwa utashindwa ikiwa hakutokuwa na mwafaka.

"Maamuzi ya kisiasa yanahitajika kutoka kwa Wairani. Ikiwa watasababisha mgogoro mkubwa katika siku zijazo, au wanakubali makubaliano ambayo yanaheshimu maslahi ya pande zote."

Mazungumzo ya mjini Vienna yanayo zijumuisha moja kwa moja nchi za Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi pamoja Marekani inayoshiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja, yalianza tena mwishoni mwa mwezi Novemba kwa lengo la kufufua mkataba wa nyuklia wa 2015. Mkataba huo ulikuwa umeipatia Tehran afueni ya vikwazo kwa sharti la kupunguza shughuli zake za nyuklia, lakini Marekani ilijiondoa mwaka 2018 na kuanzisha tena vikwazo vya kiuchumi hatua iliyosababisha Iran kuanza kujiondoa katika utekelezaji wa ahadi zake.

Iran | Videostill | Anlage zu Uran-Anreicherung in Natanz
Kiwanda cha urutubishaji Urani cha IranPicha: IRIB/AP Photo/picture alliance

Mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo Ali Bagheri Kani aliandika kupitia Twitter akisema wako karibu zaidi kuliko hapo awali kufikia makubaliano, lakini akayataka mataifa ya magharibi kuwa wakweli na kuepuka makosa ya kipindi cha nyuma.

Mapema siku ya Jumatano,Tehran ililitaka bunge la Marekani kusema nchi hiyo itawajibika ikiwa makubaliano yatafakiwa mjini Vienna. Lakini msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki anasema iwapo makubaliano hayotofikiwa katika siku zijazo basi hawatorejea katika mpango huo wa pamoja wa utekelezaji unaojulikana kama JCPOA. Soma Marekani na Iran zahimizwa kurejelea makubaliano ya nyuklia

"Kama tulivyosema hapo awali, bila shaka tutaunga mkono juhudi au fursa ya kuwa na ushirikiano wa moja kwa moja na Wairani. Tumesema kwamba lengo letu linabakia kwenye mpango ambao unaelezea masuala ya msingi ya pande zote. Na kama makubaliano hayotafikiwa katika wiki zijazo, maendeleo ya Iran ya nyuklia yatatufanya tushindwe kurejea katika mpango wa JCPOA".

Wanadiplomasia wa nchi za magharibi hapo awali walionyesha matumaini ya kuwepo na mafanikio, lakini masuala magumu bado hayajatatuliwa. Duru kadhaa zinazofuatilia mazungumzo hayo zimesema kuwa siku kadhaa zinazofuata huenda zikawa ngumu na zenye umuhimu katika kuamua ikiwa kuna mwafaka wa kufufuliwa makubaliano. Mjumbe wa China katika mazungumzo hayo Wang Qun alisema siku ya Jumatano kuwa Iran imekuwa na mwelekeo wa kujenga kwa kuweka kila kitu mezani na kufanya uamuzi wa kisiasa kwa kuzingatia njia ya kutoa na kupokea.