Uganda kuwasamehe waasi wa ADF wanaojisalimisha
31 Oktoba 2023Waziri wa habari wa nchi hiyo, Chris Baryomunsi, alisema siku ya Jumanne (Oktoba 31) kuwa maamuzi hayo yamefikiwa kwa msingi kwamba wengi wa vijana na watoto waliojiunga na waasi hao walishawishiwa kwa ahadi ambazo waasi hao wameshindwa kuzitimiza na kwamba vijana hawakuwa na nia ya kuiasi nchi yao.
Soma zaidi: Museveni alaani mauaji ya watalii
Hatua hii ya kutoa msamaha inakuja wakati majeshi ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yakiendelea na kile wanachokiita "Operesheni Shujaa" inayolenga kulitokomeza kundi hilo lenye ngome zake mashariki mwa Kongo.
Soma zaidi: Mauaji ya watalii yazusha wasiwasi Uganda
Licha ya kuorodhesha mafanikio kadhaa ya operesheni hiyo iliyoanza mwaka 2021, Rais Yoweri Museveni amekuwa akitoa tahadhari kwa wananchi kuzuia mashambulio ya kigaidi yanayopangwa na waasi wa ADF.
Wiki iliyopita, waasi hao walidaiwa kufanya mauaji ya watalii wawili wanandoa pamoja na mwongozaji wao katika mbuga ya wanyama ya Malkia Elizabeth.
Soma zaidi: Jeshi la Uganda limemuuwa kamanda wa kundi la waasi nchini Congo
Wadadisi wa masuala ya usalama na amani pamoja na wanasiasa wamepongeza hatua hiyo ya serikali kutoa msamaha malum kwa waasi hao, ila wanahimiza serikali ifanye mazungumzo na ADF ili kubaini matakwa yao na kama wanaweza kuyashughulikia badala ya kuendeleza mzozo ambao unaathiri raia wa Uganda na Kongo.