1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda na Jamhuri ya Afrika Kati Magazetini

28 Februari 2014

Operesheni Sangaris inayosimamiwa na Ufaransa katika jamahuri ya Afrika Kati kama itasaidia kuleta amani na Uganda ambako rais Yoweri Museveni ametia saini sheria kali dhidi ya watu wa jinsia moja wanaofanya mapenzi

https://p.dw.com/p/1BHVm
Rais Yoweri Museveni akitia saini sheria inayokosolewa na walimwenguPicha: Reuters

Tunaanzia Uganda ambako gazeti la Süddeutsche linazungumzia kuhusu "kuzirai" ulimwengu.Sheria hiyo mpya, linaandika gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani haithamini hadhi ya binaadamu na sababu ni waraka wa kichaa. Rais Yoweri Museveni baada ya kutia na kutoa kwa muda mrefu,ametia saini mswaada wa sheria inayotoa adhabu kali kwa watu wa jinsia moja wanaofanya mapenzi. Wanasayansi walimtanabahisha kwamba "hakuna mtu anayezaliwa na tabia hiyo". Ni watu wa kawaida tu hao,wanaofanya hivyo kwa sababu ya kutaka pesa tu". Süddeutsche Zeitung limemnukuu rais Museveni akisema.Fitna kutoka ngazi za juu zimeanza kuleta tija,siku moja baada ya rais kutia saini sheria hiyo,gazeti moja linalosomwa na wengi likachapisha wito wa kuandamwa waganda 200 wanaosemekana kuwa mstari wa mbele miongoni mwa wale watu wa jinsia moja wanaofanya mapenzi.

Süddeutsche Zeitung linazungumzia shinikizo la nchi fadhili zinazotishia kusitisha misaada yao kwa Uganda. Hata hivyo gazeti hilo linahisi misaada ya maendeleo haifai kutumiwa kushinikiza haki za binaadamu ziheshimiwe.Katika kadhia hii hata hatua ya kupunguza misaada ya maendeleo kama njia ya kuiadhibu Uganda haina maana.Waafrika wengi tokea hapo wanachoshwa na viongozi wao na wanahisi wamekuwa wakipokea amri tu kutoka nchi za magharibi.Hata wanaharakati wanaopigania haki za watu wa jinsia moja wanaofanya mapenzi wanahisi mageuzi yanabidi yaanzie humo humo nchini.Marekani kwa hivyo imemalizikia na kutangaza itachunguza upya uhusiano wake na Uganda.Hakuna mengi yanayotegemewa kutokea.Kwa sababu Marekani inaishukuru Uganda kwa kutuma wanajeshi kupambana na wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia.Linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Desmond Tutu am sihi Museveni aheshimu Haki za Binaadam

Gazeti la Neues Deutschland nalo pia limezungumzia sheria hiyo pamoja na picha na majina ya watu 200 yaliyochapishwa na gazeti la Red Pepper kuhusu wale wanaosemekana kufanya mapenzi ya jinsia moja.Limemnukuu askofu mkuu wa zamani wa Afrika kusini Desmond Tutu akiilinganisha Uganda na utawala wa wanazi wa zamani nchini Ujerumani na ule wa ubaguzi wa rangi na mtengano-Apartheid nchini Afrika kusini.Desmond Tutu amemtolea wito rais Museveni autumie mjadala uliosababishwa na sheria hiyo kuhimiza haki za binaadam na usawa nchini humo.

Zentralafrikanische Republik Bangui Alltagsleben
Shida ya maisha katika mji mkuu wa jamhuri ya Afrika kati, Bangui-watu wanasubiri mgao wa chakula kutoka shirika la umoja wa mataifaPicha: F.Daufour/AFP/GettyImages

Matumaini ya amani Jamhuri ya Afrika Kati

Lilikuwa gazeti hilo hilo la Neues Deutschland lililoandika kuhusu hofu za wananchi wa Jamhuri ya Afrika kati wanaoshuku kama opereshini Sangaris inayoongozwa na Ufaransa itasaidia kweli kurejesha amani.Neues Deutschland linasema matumizi ya nguvu yanazidi na juhudi za kuwapokonya silaha wanamgambo hazijafikia popote. Hata hivyo jarida la Der Spiegel linahisi "Bado Kuna matumaini." Der Spiegel limefanya mahojiano pamoja na rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika Kati,bibi Catherine Samba-Panza.Baada ya kuchambua shida zote zilizoko na nani wako nyuma ya makundi ya wanamgambo na dhamira zao,anakiri anasema muda mfupi madarakani hautoshi kuyapatia ufumbuzi matatizo yote yaliyoko, hata hivyo lakini ukweli kwamba yeye ni mwanamke,na kiongozi unampa moyo amini watafanikiwa.

Na hatimaye gazeti la Die Tageszeitung linalozungumzia maafa wanayokabiliana nayo wananchi wa Jamhuri ya Afrika kati.Maafa hayo yameenea hadi nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Jumla ya watu 60 elfu wameyapa kisogo maskani yao na kukimbilia upande wa pili wa mpaka katika kijiji kidogo cha wavuvi 3000 -Zongo,katika nchi hiyo jirani. Matokeo yake bei za bidhaa zimepanda na sokoni ambako zamani akinamama wakikusanyika kuuza matunda, mboga na bidhaa nyenginezo,hivi sasa sokoni kukavu.Hadi wakati huu wananchi laki mbili na nusu wa Jamhuri ya Afrika kati wameihama nchi yao na kukimbilia katika nchi jirani. Zaidi ya nusu kati yao wamekwenda Kamerun na 60 elfu katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, nchi masikini iliyoteketezwa na miaka 20 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ambayo baadhi ya wananchi wake wenyewe,watu laki mbili na nusu wanaishi katika kambi za wakimbizi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Basis/Presser/All Presse

Mhariri: Josephat Charo