1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Wafungwa zaidi ya 200 watoroka jela Karamoja

Sylvia Mwehozi
17 Septemba 2020

Jeshi la Uganda linaendesha operesheni ya kukabiliana na zaidi ya wafungwa 200 waliotoroka kutoka gereza kuu la kaskazini mashariki mwa Uganda kanda ya Karamoja Jumatano jioni.

https://p.dw.com/p/3id0l
Philippinen Manila Gefängnis Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/N. Celis

Kulingana na msemaji wa majeshi brigedia jenerali Flavia Byekwaso, wafungwa hao waliojihami kwa silaha walizowapora askari magereza wamejichimbia katika milima ya Moroto walikotorokea. 

Kulingana na takwimu za magereza, gereza kuu la Moroto lina wafungwa zaidi ya 2,000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Jumatano jioni mwendo wa saa kumi na moja, zaidi ya mia mbili kati yao waliwashinda nguvu walinzi pale walipowapokonya bunduki na kuanza kutoroka.

Mamkala ya magereza iliwaita polisi na majeshi kuwasaidia kuwakamata wafungwa hao. Jeshi liliitikia mara moja kwa kutumia ndege za helikopta na operesheni hiyo imendelea usiku kucha bila mafanikio makubwa. Akizungumza na DW kwa njia ya simu, msemaji wa majeshi brigedia Flavia Byekwaso amethibitisha taarifa hizo.

Taarifa zinaelezea kuwa wafungwa hao walivunja chumba cha kuhifadhi silaha na kutoweka na idadi ya silaha ambayo hadi sasa haijabainika lakini ni dhahiri kuwa wanatumia silaha hizo kujibu mashambulizi ya majeshi wakiwa katika milima jirani na gereza hilo walikotorokea.

Uganda Kampala City
Jiji la KampalaPicha: picture-alliance/Godong/P. Isaac

Visa vya wafungwa kutoroka katika magereza ya Uganda vimeongezeka hivi karibuni. Mwezi Machi mwaka huu wafungwa watatu waliuawa walipokuwa wakijaribu kutoroka katika gereza la Arua Kaskazini nwa mwa nchi na mwezi Julai wafungwa 11 walitoroka kutoka gereza la Bukwo Mashariki mwa nchi. Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema baadhi ya sababu za mwenendo huu ni msongamano mkubwa katika magereza hayo.

Kutoroka kwa wafungwa huko Uganda

Takwimu zinaonyesha kuwa magereza ya nchi yana asli mia 300 ya uwezo wake. Aidha kufuatia janga la COVID-19 wafungwa wengi kupitia kwa mawakili wao, wamekuwa wakilalamikia uwezekano wa kuambukizwa kutokana na msongamano huo. Msemaji wa magereza alizungumzia suala hilo hapo kabla.

Hata hivyo, msemaji huyo wa magereza hakupatikana kuzungumzia kisa hicho cha wafungwa wengi kutoroka kutoka katika gereza hilo la Moroto ambapo wafungwa 30 waligunduliwa kuwa na virusi vya COVID-19 wiki iliyopita.

Lubega Emmanuel DW Kampala.