Wanachama wa upinzani FDC Uganda washtakiwa kwa ugaidi
30 Julai 2024FDC ni miongoni mwa vyama vikubwa vya kisiasa nchini Uganda kinachoongozwa na Dkt Kizza Besigye, mwanasiasa mkonwe wa upinzani nchini humo ambaye amewahi kugombea urais mara nne.
Wakili wao, Erias Lukwago, amewaambia waandishi wa habari nje ya mahakama mjini Kampala kwamba watu hao walikamatwa nchi jirani ya Kenya katika mji wa Kisumu, walikokuwa wamekwenda kushiriki warsha kuhusu uongozi na kwamba mashtaka yanayowakabili wateja wake hayana msingi.
Soma pia: Polisi nchini Uganda yawakamata waandamanaji 104
Kulingana na taarifa za mashtaka watu hao walikwenda kupata mafunzo ya kigaidi na kwa kuwa hawakuwa na mwenyeji rasmi nchini Kenya, polisi ya Kenya iliwasiliana na vyombo vya usalama vya Uganda kabla ya kuwakamata na kisha kusafirishwa nchini Uganda.
Dkt Kizza Besigye ameikosoa hatua hiyo ya kukamatwa wafuasi wa chama chake na kuulaumu utawala wa Kenya kwa kufanya hila.
Wafuasi hao 36 wa FDC wakiwemo wanawake watatu wamepelekwa rumande hadi tarehe 13 mwezi Agosti.