1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yathibitisha kukamatwa kwa Lawrence Muganga

Lubega Emmanuel 3 Septemba 2021

Msemaji wa jeshi la Uganda amethibitisha kushikiliwa mjini Kampala makamu wa chansela wa chuo kikuu cha Victoria,Lawrence Muganga kwa tuhuma za ujasusi.

https://p.dw.com/p/3ztHD
Uganda Polizei
Picha: Zuma Press/Imago Images

Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Flavia Byekwaso amethibitisha kuwa wanamshikilia makamu wa chansela wa chuo kikuu cha Victoria cha mjini Kampala kwa madai ya kulifanyia ujasusi taifa la kigeni.

Awali palikuwa na madai kwenye mitandao ya kijamii kuwa msomi huyo Dkt. Lawrence Muganga ambaye inadaiwa ni raia wa Rwanda pamoja na msaidizi wake walikuwa wametekwa nyara na watu wasiojulikana.

Kanda ya vidio inayoonyesha makamu wa chansela wa chuo kikuu cha Victoria Dkt Lawrence Muganga akikamatwa na kuburutwa kwa mabavu na watu waliovalia nguo za kiraia ndilo gumzo linalotawala kwenye majukwaa mbalimbali. Taharuki ya kisa hicho iliyokumba wafanyakazi wa chuo hicho kilichoko katikati ya mji wa Kampala awali  ilidhaniwa kuwa ni utekaji nyara. Baada ya polisi kukanusha kuhusika katika kisa hicho, msemaji wa majeshi Brigedia Flavia Byekwaso ametoa ufafanuzi kuwa operesheni ya kumkamata msomi huyo iliendeshwa na maafisa wa upepelezi wa jeshi kwani anadaiwa kuhusika katika masuala ya ujasusi kwa niaba ya taifa la kigeni. 

Msemaji wa majeshi aidha amefahamisha kuwa bwana huyo ana hati ya usafiri ya kigeni na mke wake ana paspoti ya Rwanda na wamekuwa wakiishi Uganda na kufanya kazi kinyume na sheria. Kulingana na maoni ya watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kwa mara nyingine vyombo vya usalama vilikiuka haki za binadamu za bwana huyo wakati waliomkamata  msomi huyo walipotumia nguvu za kupindukia huku wakiwa wamejihami kwa bunduki.

Maslahi za kisiasa ?

Demonstranten Studenten der Makerere Universität in  Uganda
Picha: picture alliance/AA/L. Abubaker

Dkt. Lawrence Mganga ambaye alizaliwa na kusomea Uganda aliwahi kwenda Rwanda kufanya kazi za kutoa ushauri kwa makampuni yaliyokuwa yakianza shughuli zao na kisha alikwenda kwa masomo zaidi Canada. Kulingana na msemaji wa majeshi ana kitambulisho kinachonyesha kuwa ni raia wa Canada.Yeye ni miongoni mwa kundi la watu wa jamii ya Banyarwanda ambao wametaka watambuliwe kuwa Bavandimwe ili waondokane na manyanyaso na kunyimwa haki kama raia wa Uganda wakidaiwa kuwa ni raia wa Rwanda. Frank Gashumba ambaye ni mmoja kati ya viongozi wa vuguvugu hilo la Bavandimwe anahoji kwa nini makachero wa kijeshi hawakufuata utaratibu wa kisheria kumkamata bwana huyo.

Dkt Muganga ni miongoni mwa jamii ya Wanyarwanda ambao wazazi wao walikimbilia Uganda miaka ya 1950 lakini kumekuwepo mvutano kati ya kundi hio na lile la Wanyarwanda ambao walibaki kwa upande wa Uganda wakati mipaka kati ya nchi hizi mbili ilipochorwa na wakoloni. Kisa hiki kinavuta tena mjadala kuhusu mzozo kati ya serikali ya Uganda na ile ya Rwanda, Uganda ikidai kwa Rwanda huwatuma majasusi kufuatilia mambo yake ya ndani ya Uganda.