1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki iko tayari kwa mazungumzo kutatua mvutano na Uturuki

Sylvia Mwehozi
25 Agosti 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki Nikos Dendias amesema taifa hilo liko tayari kufanya mazungumzo ili kutatua tofauti zake na Uturuki wakati mataifa hayo mawili yakitangaza kufanya mazoezi pinzani ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/3hUbf
Griechenland | Bundesaußenminister Heiko Maas und Nikos Dendias
Picha: Getty Images/AFP/Eurokinissi/STR

Uturuki na Ugiriki zimetangaza mazoezi pinzani ya kijeshi katika eneo la Mashariki mwa Mediterenia wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas akisema hali inayoendelea ni sawa na kuchezea moto. 

Tangazo hilo kutoka kwa Ugiriki na Uturuki linazidisha mvutano juu ya madai ya rasilimali ya mafuta kwenye eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterenia. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Heiko Maas ambaye anazitembelea nchi hizo mbili, tayari amewasili Athens, Ugiriki na kukutana na waziri mwenzake Nikos Dendias.

Maas amesema hali iliyopo sasa katika eneo linalozozaniwa ni sawa na kuchezea moto, na kwamba kila cheche ndogo inaweza kuchochea janga kubwa na hakuna mwenye maslahi ya makabiliano ya kijeshi baina ya washirika wa Jumuiya ya kujihami NATO na majirani zake. Zaidi anasema ;

''Nimekuja hapa leo na ujumbe wa aina mbili ambao wote una umuhimu mkubwa. Ujumbe wa kwanza ni kwamba Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa pamoja zinasimama na Ugiriki kwa mshikamano mkubwa. Na ujumbe wa pili ambao una umuhimu sawa ni kile kinachohitajika kwa haraka, viashiria vya kupunguza mvutano na utashi wa kushiriki mazungumzo.''

türkischer Bohrschiff Yavuz
Meli ya Uturuki ikisindikizwa na meli nyinginePicha: Reuters/M. Sezer

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki, Nikos Dendias amemueleza Maas kwamba taifa hilo liko tayari kushiriki mazungumzo ya kutatua mzozo na Uturuki, lakini akasisitiza kwamba watalinda haki zao. ''Tunavyozungumza hivi sasa Uturuki inaendelea kuvunja sheria, kuzidisha mvutano na uchokozi, licha ya wito unaotolewa na majirani, pande zote na washirika,'' amesema waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ugiriki.

Waziri huyo amesema suala hilo si tu linawatia wasiwasi washirika wawili wa NATO, bali pia Umoja wa Ulaya kwa ujumla. Mara baada ya kuitembelea Athens waziri Maas ameelekea Ankara siku ya Jumanne kuendelea na juhudi za kuutatua mvutano.

Ujerumani iliingilia kati mzozo huo mwezi uliopita na kusababisha Uturuki kusitisha kwa muda operesheni zake kwa ajili ya mazungumzo na Ugiriki. Baada ya Ugiriki na Misri kufikia makubaliano ya kuweka mipaka ya baharini ingawa Uturuki iliendelea na operesheni zake.

Ugiriki imekuwa mara kwa mara ikiutaka Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Uturuki kutokana na shughuli zake, wakati Uturuki yenyewe ikiutolea wito umoja huo kuacha kuikumbatia Ugiriki na badala yake ishinikize majadiliano. Hadi kufikia Jumanne meli ya Uturuki ya Oruc Reis ambayo inafanya utafiti ilikuwa katikati ya Cyprus na Crete. Siku ya Jumapili Uturuki ilitoa taarifa ya Navtex ya upanuzi wa operesheni ya meli zake hadi Agosti 27, huku Ugiriki nayo ikitoa taarifa kama hiyo ya kufanya mazoezi ya kijeshi kwa siku tatu kwenye eneo hilo hilo nje ya kisiwa cha Ugiriki cha Crete.