1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yahofia watu 500 wamekufa kwenye ajali ya boti

15 Juni 2023

Mamlaka nchini Ugiriki zimesema zinaamini kuwa zaidi ya watu 500 wamekufa baada ya boti ya wahamiaji kuzama.

https://p.dw.com/p/4ScNK
Griechenland | Schiffsunglück bei Kalamata
Picha: Eurokinissi/REUTERS

Mamlaka nchini Ugiriki zimesema zinaamini kuwa zaidi ya watu 500 wamekufa baada ya boti ya wahamiaji kuzama hapo jana kwenye maji ya kina kirefu umbali wa kilometa 90 kutoka pwani ya nchi hiyo.

Tathmini hiyo inatokana na simulizi za manusura wa mkasa huo ambao baadhi yao wamekadiria kwamba boti hiyo huenda iliwabeba zaidi ya watu 700 ikiwemo watoto wanaofikia 100.

Hadi sasa ni miili 78 pekee ndiyo imepatikana na watu wengine 104 wameokolewa katika operesheni iliyoendeshwa na walinzi wa pwani ya Ugiriki kutwa nzima ya leo. Inaaminika boti hiyo ya uvuvi iliianzia safari yake nchini Libya kuwapeleka mamia ya wahamiaji barani Ulaya.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametuma salamu za rambirambi na kuomboleza vifo vilivyotokana na mkasa huo unaotajwa kuwa ndiyo mbaya zaidi kuwahi kutokea miaka ya karibuni barani Ulaya.