Ugiriki yaomba msaada kutoka Ulaya na IMF
24 Aprili 2010Waziri wa Fedha wa Ugiriki, George Papaconstantinou amesema msaada wa fedha kutoka nchi za kanda ya Euro na shirika la fedha la kimataifa , IMF upo njiani lakini utachukua siku kadhaa kabla ya kufika nchini humo.
Siku ya Ijumaa, Ugiriki ilitoa ombi kwa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, kuipatia msaada wa Euro bilioni 45 ili iweze kulipa madeni yake makubwa.
Lakini Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema, kuna masharti ya kutimizwa. Kwanza, mpango unaoaminika kupunguza matumizi, ujadiliwe kati ya Ugiriki, Kamisheni ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa. Pili, mpango huo utakapowasilishwa, basi Kamisheni ya Ulaya, Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa lazima zitathmini ikiwa hali ya sarafu ya Euro inalazimisha kuisaidia Ugiriki."
Baada ya kutimizwa kwa masharti hayo mawili, masuala mengine kuhusu kiwango na njia ya kutoa msaada huo yanaweza kujadiliwa.
Mwandishi:Moss,Peter/RTRE/AFP
Mhariri:Martin,Prema