Ugiriki yapiga kura, euro mashakani
17 Juni 2012Wagombea wakuu, chama cha kihifidhina cha New Democracy na Syriza chama cha nadharia za mrengo wa kushoto, vimeahidi kila kimoja kuunda serikali ambayo itajadili upya masharti magumu ya mkopo wa kuiokoa nchi hiyo uliotolewa na umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF, lakini wanataka kufanya hivyo kwa masharti yao binafsi.
Tatizo ni kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni yaliyopita na kuchapishwa mapema mwezi huu, hakuna chama kitaweza kuongoza bila ya kuwa na washirika , na kuunda hata serikali yenye muungano usio imara ni suala ambalo halina uhakika, wanasema wa wadadisi wa masuala ya kisiasa.
Serikali ya mseto
Iwapo chama cha New Democracy ni chama cha kwanza , uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ni rahisi kuliko iwapo chama cha kwanza kitakuwa Syriza, amesema vassiliki Georgiadou, mhadhiri wa sayansi ya kisiasa katika chuo kikuu cha Panteion mjini Athens.
Lakini hali zote sio rahisi, amesema.
Amesema serikali ya mseto inapaswa kuhusisha vyama vitatu ili kuwa imara, ambapo chama cha Kisoshalist cha Pasok na chama cha Democratic ambacho kinaonekana kuwa kitaweza kuwa chama kitakachotawaza kiongozi wa serikali.
Ameongeza kuwa hali hiyo inatakiwa kuidhinishwa na wapigakura. Serikali yoyote itakumbana na hali ngumu ya kuweka uwiano kati ya matakwa ya umma ya kutaka kupunguzwa kwa hatua za kubana matumzi zilizowekwa katika muda wa miaka miwili iliyopita na msisitizo wa wakopeshaji wa umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa, kuwa Ugiriki ni lazima iendelee na mpango huo.
Msaada wa kimataifa
Ugiriki tayari imelazimika kuomba msaada mara mbili wa uokozi, wa kwanza ukiwa na thamani ya euro bilioni 110 katika mwaka 2010 na tena euro bilioni 130 mwaka huu pamoja na kufutwa kwa deni la watu binafsi lenye thamani ya euro bilioni 107, ikiwa ni jumla ya euro bilioni 347.
Kiongozi wa chama cha Syriza Alexis Tsipras mwenye umri wa miaka 31 ameahidi kufuta makubaliano ya uokozi na tayari amekataa kushirikiana na chama cha New Democracy ama kile cha Pasok , vyama ambavyo vimeshiriki katika kuiongoza nchi hiyo katika muda wa miongo minne iliyopita.
Karamu ya rushwa
Tspras amevishutumu vyama vyote viwili kwa kuitumbukiza nchi hiyo katika kile alichokieleza kuwa ni hafla ya rushwa, katika miaka vilivyokuwa madarakani na ameahidi kukomesha mfumo huo wa uoza.
Antonio Samaras mwenye umri wa miaka 61 ,ambaye ni mkubwa wake kiumri , amebeua ahadi za chama cha Syriza za kurejesha mishahara kama zamani, kuwa ni uchumi wa vitabu vya vichekesho.
Umma, pamoja na hali halisi vinadai kuwa serikali ni lazima iundwe. Haiwezekani kuendelea zaidi zaidi ya hapa, amesema kiongozi wa chama cha New Democracy Samaras hapo kabla.
Wakati huo huo mkuu wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo katika bara la Ulaya OECD, Angel Gurria amesema kuwa Ugiriki inapaswa kupewa nafasi ya kujadili upya masharti ya mpango wa kimataifa wa uokozi wenye thamani ya euro bilioni 130, iwapo hii itakuwa na maana ya kuibakisha nchi hiyo katika eneo linalotumia sarafu ya euro.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri : Sudi Mnette