1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yasafirisha kundi la pili la wahamiaji

Yusra Buwayhid8 Aprili 2016

Ugiriki imesafirisha kundi la pili la wahamiaji 45 kwenda Uturuki, chini ya makubaliano ya Umoja wa Ulaya yenye utata. Wakati Ujerumani ikisema idadi ya wahamiaji wanaomba hifadhi nchini imepungua kwa asilimi 66

https://p.dw.com/p/1IRo8
Griechenland Flüchtlinge auf Lesbos
Picha: Getty Images/M. Bicanski

Wahamiaji hao 45 wote raia wa Pakistani, waliondoka kisiwa cha Lesbos cha Ugiriki kupitia feri litakalowasafirisha hadi Uturuki. Huku kundi lengine la wahamiaji 80 likiwa linategemewa kusafirishwa baadae leo hii.

Wanaharakati watatu walikamatwa na polisi baada ya kujitumbukiza majini na kuishikilia nanga ya feri hilo, wakiwa wanajaribu kulizuia kuondoka. 30 wengine walikusanyika katika bandari ya kisiwa hicho, wakipinga kusafirishwa kwa wahamiaji hao.

Kundi la mwanzo la wahamiaji 202 lilisafirishwa na kupelekwa Uturuki kutoka visiwa vya Lesbos na Chios Jumatatu iliyopita. Hatua hiyo ilizua kiwewe cha kujiandikisha kuomba hifadhi, miongoni mwa wahamiaji. Na kupelekea mamlaka za Ugirki kuchelewesha uhamishaji zaidi wa wahamiaji, kutokana na kukabiliwa na kazi ya kushughulikia kesi moja moja ya watu hao waliomba hifadhi. Lakini kulingana na serikali ya Ugiriki, mchakato huo unawahusu wale wahamiaji waliokuwa hawakuomba hifadhi rasmi kutoka Ugiriki.

Hofu ya kusafirishwa imewafanya wengi wao kukata tamaa, wahamiaji kadhaa katika visiwa vya Samos na Lesbos inasemekana wameanza mgomo wa chakula, kama njia ya kuishinikiza Ugiriki kuachana na mpango wa kuwapeleka Uturuki. Badala yake wanachokidai ni kufunguliwa kwa mipaka ya mataifa ya Balkan iliyofungwa mwezi uliopita, ili waendelee na safari yao ya kuelekea nchi za kaskazini mwa bara la Ulaya ikiwamo Ujerumani.

Wanaomba hifadhi wamepungua kwa asilimia 66 Ujerumani

Deutschland Konferenz zu Gewalt gegen Beschäftigte im öffentlichen Dienst
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Aidha Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema, kwa mwezi Machi pekee idadi ya wahamiaji wanaomba hifadhi nchini humo imepungua kwa asilimia 66, hadi kufikia wahamiaji 20,000.

Chini ya masharti ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, wahamiaji haramu waliowasili nchini Ugiriki tokea Machi 20 mwezi uliopita watarejeshwa walipotoka, ingawa makubaliano hayo pia yanalazimisha kila kesi ishughulikiwe kikamilifu kabla ya mhamiaji kusafirishwa.

Mwaka jana Ujerumani ilipokea zaidi ya wahamiaji milioni moja, baada ya kansela wa Angela Merkel kuwafungulia milango wahamiaji bila ya kuzingatia sheria za kutoa hifadhi za Umoja wa Ulaya.

Aidha kulingana na makubaliano hayo, kwa kila mhamiaji atakaerejeshwa Uturuki, mkimbizi kutoka Syria atasafirishwa kutoka Uturuki kwenda barani Ulaya kwa njia halali na salama, kikomo kikiwa ni wakimbizi 72,000.

Kwa kuyafanya hayo Uturuki imeahidiwa mambo kadhaa na Umoja wa Ulaya, ikiwamo raia wake kuweza kusafiri bila ya kutumia visa barani Ulaya, kuanzia Juni mwaka huu.

Aidha rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameutahadharisha Umoja huwo kwamba nchi yake haitotekeleza makubaliano ya kuipunguzia Ugiriki wahamiaji kikamilifu, iwapo kwa upande wao watashindwa kutimiza ahadi zao kwa Uturuki.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre

Mhariri: Daniel Gakuba