Maandamano ya Pegida yazingatiwe
14 Januari 2015Uhuru wa mtu kutoa maoni yake,na nini cha kufanya kuondoa chuki katika jamii,yakizingatiwa mashambulio ya kigidi ya Paris na maandamano ya kundi linalopinga kuenezwa dini ya kiislam katika nchi za Ulaya ni miongoni mwa mada zilizopewa umbele na magazeti ya Ujerumani.
Tuanzie lakini na alifu yaani :Uhuru wa mtu kutoa maoni yake. "Saarbrücker Zeitung" linaandika:"Tangu jumapili iliyopita,mamilioni ya watu wamekuwa wakiteremka majiani mijini Paris,Saarbrücken,Leipzig na Berlin kudai uhuru wa mtu kutoa maoni yake pamoja na uvumilivu.Kwa mtazamo wa ndani na nje, hilo ni jambo muhimu na la maana.Cha kuvutia ni kwamba katika mji wa Leipizig serikali iliruhusu mabango yanayotusi au kuikashifu dini,naiwe ya kiislam au nyengine-kwasababu ya uhuru wa mtu kutoa maoni yake.Hilo lakini lisiwe la upande mmoja-linaabidi lifuate fikra ya Rosa Luxemburg:katika kila jamii huru,kuna uhuru wa wenye maoni tofauti pia .
Uhuru wa mtu kutoa maoni yake na nini cha kufanya kukabiliana na kishindo kinachotokana na maandamano ya kundi la "wazalendo wanaopinga kuenezwa dini ya kiislam barani Ulaya "Pegida"?,linajiuliza gazeti la "Rhein-Zeitung":"Kimoja tu ndicho kitakachosaidia:"Maelezo."Wanasiasa wanabidi hatimae wasikilize kile kinachowapasua vichwa wananchi, kuanzia majumbani,mikahawani na kwengineko.Wanabidi waelewe hofu na wasi wasi wa wananchi zinapohusika sera za wakimbizi na wawaeleze wapi hofu zao hazina msingi.Wanabdi wawashirikishe wakaazi wa miji na mitaa maamuzi yanapopitishwa kuhusu wapi wapelekwe wakimbizi na sababu kufafanuliwa.Na wanabidi hatimae pia watambue wakati gani hofu na wasi wasi wa wananchi ni wa msingi na wapi wanasiasa wanabidi kuingilia kati.Anaeamini kwamba kuwaandama Pegida pekee kunatosha,anakosea."
Gazeti la "Freie Presse" linahisi ingekuwa vyema kama wanasiasa wangezungumza na Pegida.Gazeti linaendelea kuandika:"Wanasiasa wameshagundua hali namna ilivyo.Wanataka kusaka mazungumzo pamoja na wananchi.Majadiliano pamoja na PEGIDA hakuna.Na mpaka sasa hakuna hata mwakilishi mmoja wa vyama vikuu aliyejaribu kuwasiliana na waasi wa vuguvugu hilo.Lakini ukweli ni kwamba watu wanabidi wazungumze nao.Wanaandaa maandamano na waandamanaji wanawathamini na kuwataja kuwa ni wawakilishi wao.Hata kama si rahisi,lakini wakuu wa makundi ya vyama vinavyowakilishwa bungeni wanabidi wapige moyo konde.Kwasababu amani ya jamii ndiyo inayotishia kuingia hatarini nchini mwetu."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Josephat Charo