1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza imesitisha safari ya waomba hifadhi kwenda Rwanda

15 Juni 2022

Uingereza imesitisha safari ya ndege ya kwanza ya waomba hifadhi iliyokuwa imepangwa kufanyika Jumanne, baada ya Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya kusema mpango huo unaakisi athari zisizoweza kurekebishwa.

https://p.dw.com/p/4CiII
UK | Abschiebeflug nach Ruanda
Picha: Dan Kitwood/Getty Images

Uamuzi huo ni baada ya siku kaadhaa za vita nikuvute za kisheria kutoka kwa mawakili wenye kupigania haki za binaadamu, ambao walianzisha mfululizo wa rufaa zenye lengo la kuzuia hatua ya ufukuzwaji watu katika orodha ya serikali.

Awali hapo jana maafisa wa serikali ya Uingereza walisema ndege hiyo ingeanza safari yake bila ya kujali itakuwa na abiria wangapi ndani. Lakini baada ya rufaa hizo hakuna aliyesalia. Ijumaa iliyopita vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa watu ambao walipaswa kuondoshwa nchini humo walikuwa zaidi ya 30.

Uingereza inajipanga upya kwa safari nyingine.

Großbritannien Protest gegen die Abschiebung von Geflüchteten zurück nach Ruanda
Wapinga kuondishwa kwa wahamiaji nchini UingerezaPicha: Niklas Halle'n/AFP/ Getty Images

Baada ya kusitishwa kwa safari hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel alisema amesikitishwa lakini hana uwezo wa kuzuia haki kutendeka. Hata hivyo amesema timu ya wanasheria ya serikali inapitia kwa kina uamuzi huo na kujiandaa safari nyingine ya ndege.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliyekuwa akiukingia kifua mpango huo wa Uingereza anasema kuwa ni njia halali ya kulinda maisha ya watu na kuzuia magenge ya wahalifu ambayo husafirisha wahamiaji kwa kutumia ujia wa bahari wa Uingereza kwa kutumia boti ndogo.

Katika miaka ya hivi karibuni Uingereza imeshuhudia idadi kubwa ya wimbi la wakimbizi kutoka maeneo kama vile Syria, Afghanistan, Iran, Sudan, Iraq na Yemen.

Makubaliano ya serikali za Uingereza na Rwanda

Johnson alitangaza makubaliano na Rwanda mwezi Aprili ambapo watu wanaoingia Uingereza kinyume cha sheria watalazimishwa kupelekwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Kwa hatua hiyo, Rwanda itapokea mamilioni ya pauni  kwa ajili ya misaada ya maendeleo.

Wahamiaji hao watapaswa kuomba hifadhi wakiwa Rwanda na sio Uingereza.  Wanaoipinga hatua hiyo wanasema ni kinyume cha sheria na ni kitendo cha kinyama, kwa kuwapeleka watu katika taifa la mbali na pia nchi ambayo wasingependa kuishi.

Viongozi wa Kanisa nchini Uingereza walijiunga na upande wa upinzani kukipinga kitendo hicho kwa kukiita kuwa ni sera ya serikali isiyo ya maadili, juhudi ambayo imeungwa mkono pia Mwanamfalme Charles kwa mujibu wa duru za habari za Uingereza. Kadhalika wanaharakati wameshutumu sera hiyo kama shambulio dhidi ya haki za wakimbizi ambao nchi nyingi zimewatambua tangu mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Soma zaidii: Uingereza kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi wa kwanza

Wakati Uingereza ilipokuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ilikuwa sehemu ya mfumo wenye kufanikisha wakimbizi kuomba hifadhi katika sehemu ya kwanza salama wanayoingia. Lakini ilipoteza nafasi hiyo baada ya kujiondoa katika muungano wa mataifa hayo.

Chanzo: AP