1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Uingereza na washirika washambulia waasi ya Kihouthi Yemen

24 Januari 2024

Uingereza imesema kuwa nchi 24, ikiwemo Marekani, Ujerumani na Australia zimefanya mashambulizi ya anga kuyalenga maeneo manane yanayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/4bcLi
Mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi, Yemen
Vikosi vya nchi 24 vikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Kihouthi, YemenPicha: CENTCOM/Anadolu/picture alliance

Taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumanne na ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak imeeleza kuwa katika kujibu mashambulizi yanayoendelea ya waasi wa Kihouthi, dhidi ya meli zinazopita katika Bahari ya Shamu na njia zinazoizunguka bahari hiyo, vikosi vya jeshi vya Marekani na Uingereza vikiungwa mkono na Australia, Bahrain, Canada, Uholanzi na New Zealand, vimefanya mashambulizi ya ziada kwenye maeneo yanayokaliwa na waasi hao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi hayo yalianzishwa kwa lengo la kuvuruga na kuudhofisha uwezo wa waasi wa Kihouthi kuendeleza mashambulizi yao dhidi ya biashara ya kimataifa na mabaharia wasio na hatia kutoka ulimwenguni kote, bila kuchochea makabiliano na waasi hao.

Waziri Mkuu Sunak amesema waasi wa Kihouthi wanaendelea kuleta kitisho cha mara kwa mara kwa meli za kibiashara kwenye Bahari ya Shamu.

Uingereza yafanya mashambulizi ya pili ya anga dhidi ya Wahouthi

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi SunakPicha: Jessica Taylor/UK Parliament/AFP

Matamshi hayo ameyatoa wakati ambapo Uingereza imeanzisha mashambulizi yake ya pili ya anga dhidi ya waasi hao. ''Mashambulizi yalielekezwa kwenye maeneo tunayoyalenga tu na tumechukua tahadhari ya juu kuwalinda raia,'' alifafanua Sunak.

Kwa mujibu wa Sunak, tayari wameshadungua makombora na droni kadhaa ambazo zilizilenga meli za kiraia na kwamba wanaendelea kushirikiana kidiplomasia kwa sababu wanatambua wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu ugumu wa hali iliyopo sasa.

Soma zaidi: Maeneo ya Wahouthi yashambuliwa tena Yemen

Sunak amedai kuwa waasi wa Kihouthi wamefanya mashambulizi zaidi ya 12, tangu duru ya kwanza ya mashambulizi ya pamoja ya Januari 11.

Huku hayo yakijiri, Urusi imeuambia Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihouthi, yanatishia amani ya kimataifa.

Akizungumza mjini New York, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amelaani vikali mashambulizi yanayofanywa na Marekani na Uingereza kwa kusaidiwa na washirika wake dhidi ya waasi hao wa Yemen.

Lavrov: Mashambulizi hayo ni kitisho kwa amani ya kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov Picha: SNA/IMAGO

Lavrov amesema mashambulizi hayo ni "uchokozi usio na msingi" na kitisho cha moja kwa moja kwa amani ya kimataifa.

Wakati huo huo, mabalozi walioko nchini Yemen kutoka katika nchi tano ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatarajia kukutana Jumatano kuzungumzia hali inayoendelea nchini Yemen.

Shirika la habari la serikali ya Urusi, TASS limeripoti kuwa wanadiplomasia hao kutoka Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani watakutana licha ya utata wa hali iliyopo hivi sasa ulimwenguni. Balozi wa Urusi nchini Yemen, Evgeny Kudrov ameiambia TASS katika mahojiano kwamba mkutano huo utafanyika Januari 24, na wataendelea kubadilishana mawazo kwa njia ya mikutano ya mara kwa mara ya mabalozi hao nchini Yemen.

(DPA, Reuters)