Uingereza yasusia mkutano wa Kampala wa Jumuiya ya Madola
4 Januari 2024Akifungua rasmi kongamano hilo la siku nne, Rais Museveni ametoa angalizo kuwa ijapokuwa mataifa yaliyokuwa makoloni hasa ya Uingereza yalikubali kuwa na chombo kama cha Jumuiya ya Madola, haimaanishi kwamba Uingereza na washirika wake wa Magharibi wana haki ya kuyashinikiza mataifa ya jumuiya hiyo kuendeleza kasumba na itikadi zao. Amesema hayo ni mataifa huru yanayofanya maamuzi kwa ajili ya msingi wa maslahi ya watu wao.
''Acheni kututawala kwa hila na ujanja. Mkidhani mko sawa mnaweza kutushawishi kwa kuwa mifano kwetu.'', alionya Museveni.
Uingereza na Canada ni wanachama muhimu wa Jumuiya ya Madola yenye nchi 56 wanachama, ila hakuna wajumbe waliotokea nchi hizo ambao wanashiriki katika kongamano hilo. Ni kwa msingi huu ndipo Spika wa Bunge la Kenya Moses Wetangula amehoji kwa nini Uingereza iendelee kuhusishwa katika makongamano ya Jumuiya ya Madola huku ikichochea uhasama miongoni mwa mataifa ya jumuiya hiyo.
''Uingereza imechochea kususiwa kwa kongamano hili na mataifa fulani. Hata kama hatukubaliani kwa masuala fulani, ni jambo la busara tukutane tukubaliane au tutofautiane. Nchi iliyochochea kususia isipewe fursa ya kuwa mwenyeji wa kongamano hili.'', alisema Wentangula.
''Ni muhimu kwa kila taifa kuheshimu taifa lingine''
Kutohudhuria kwa Uingereza na Canada kumetafsiriwa na baadhi ya wabunge wa Uganda kuwa ishara ya mataifa hayo kuonyesha kero yao kuhusu sheria dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja iliyopitishwa na Uganda. Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson, ameelezea kwa nini ni muhimu mataifa yote kuheshimu sheria na itikadi za mataifa mengine.
''Ni muhimu kwa kila taifa kuheshimu taifa lingine kwa ujumla wake. Iwapo kuna taifa ambalo halijafanya sawa, basi tufuate sheria za kimataifa.''
Spika huyo wa Bunge la Tanzania ameendelea kuelezea kwa undani umuhimu wa kongamano hilo.
''Jambo litakalozungumziwa hapa ni la mazingira kwa maana ya tabianchi, lingine ni kuangalia namna mabunge yetu yanaweza kuzisaidia nchi zetu kulinda mazingira ambapo kila kundi katika jamii lina uwakilishi.''
Kongamano la 27 la Maspika wa mabunge wa Jumuiya ya Madola
Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among amewashukuru wajumbe waliokubali mwaliko wa kuhudhuria kongamano hilo akisema kuwa ni muhimu kwa watu wapatao bilioni 2.4 wa Jumuiya ya Madola wanaotarajia mabunge yao kukuza na kuendeleza demokrasia na utawala wa kisheria.
Kongamano la maspika wa mabunge wa Jumuiya ya Madola pamoja na maafisa wanaoendesha shughuli za mabunge hufanyika kila baada ya miaka miwili, na kongamano hilo lilianza kufanyika kwa mara ya kwanza nchini Canada mwaka 1969. Na kwa awamu ya 27 ya kongamano hilo kwa mwaka huu, inafanyika hapa nchini Uganda.