Ujerumani haitoiacha Afghanistan mkono! asema,Westerwelle.
10 Januari 2011Kiongozi huyo amewatembelea wanajeshi wa Ujerumani wanaopiga doria kwenye eneo la kaskazini mwa Afghanistan. Wakati huo huo Waziri Westerwelle ameahidi kuusadia uongozi wa Afghanistan katika harakati zake za kuwadhibiti wanamgambo.Akiwa katika ziara yake hiyo iliyodumu kipindi cha saa tatu, Waziri wa Mambo ya Nje Guido Westerwelle na naibu Kansela wa Ujerumani waliwasifu wanajeshi hao kwa kuyahatarisha maisha yao ili kuulinda uhuru na usalama. Waziri Westerwelle anatarajiwa pia kukutana na gavana mpya wa jimbo la Kunduz, Muhammad Anwar Jegdalek, aliyechaguliwa baada ya mtangulizi wake kuuawa mwezi wa Oktoba mwaka uliopita.
Mashada ya kumbukumbu
Kiongozi huyo anatazamiwa pia kuweka shada la maua kama kumbukumbu ya wanajeshi wa Ujerumani waliouawa wakipiga doria.
Hapo jana alikutana na rais wa Afghanistan Hamid Karzai na kwa pamoja walitoa wito wa kuyaimarisha mapambano dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya na ufisadi vilevile kuyalinda makundi madogo ya kidini.
Ziara hii inafanyika wakati ambapo Bunge la Ujerumani linasubiriwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu kuiamua hatma ya majukumu ya wanajeshi wake wanaopiga doria Afghanistan. Endapo bunge litaridhia, wanajeshi hao wataanza kuondoka Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopendekezwa baada ya kuyazingatia mazingira yaliyopo. Waziri Westerwelle anaeleza kuwa,''Mwaka wa 2011 ndio utakaoiamua hatma ya suala hilo la Afghanistan kwani ndipo mchakato mzima wa kuyakabidhi majukumu ya usimamizi wa usalama utakapoanza.''
Afghanistan kuungwa mkono
Uamuzi huo wa bunge pia utaiidhinisha hatua ya kuiongeza idadi ya wanajeshi waliopo Afghanistan kutoka 4,415 hadi 5350. Wengi ya wanajeshi hao wanapiga doria katika eneo la Kunduz. Kwa upande wake Waziri Westerwelle alisema kuwa ana imani Bunge litayaidhinisha mapendekezo hayo. Hata hivyo alisisitiza kuwa ,'' Ujerumani kamwe haitoiacha Afghanistan katika miaka ya baada ya 2014, tutaendelea kuutimiza wajibu wetu kwani azma yetu ni kufanikiwa wala sio kuyatelekeza majukumu yetu ya kiusalama katika mapambano dhidi ya ugaidi,'' kama njia ya kupambana na ugaidi.
Vikosi vya ISAF
Waziri Westerwelle alikuwa akitokea Pakistan alikotoa wito wa ushirikiano zaidi katika vita dhidi ya ugaidi na kwamba mchango wa Pakistan una umuhimu mkubwa. Mapigano yanaripotiwa kuongezeka katika eneo la kaskazini mwa Afghanistan hasa baada ya vikosi vinavyosimamiwa na ISAF chini ya mwamvuli wa NATO kwa ushirikiano na wanajeshi wa Afghanistan wameziimarisha harakati zao za kupambana na uasi.
Ili kulithibitisha hilo hapo jana jioni wapiganaji wa Taleban walipambana na wanajeshi wa NATO na Afghanistan katika mkoa wa Dasht-e-Archi, shambulio lililowaua wapiganaji 15 na kamanda mmoja.
Vikosi hivyo vya Jumuiya ya Kujihami ya mataifa ya magharibi NATO itaanza rasmi kuyakabidhi majukumu ya usalama kwa wanajeshi wa Afghanistan mwaka huu. Mchakato huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2014.
Mwandishi: Mwadzaya,Thelma-DPAE/RTRE
Mhariri:Josephat Charo