Ujerumani kupiga marufuku shughuli zote za Hamas
12 Oktoba 2023Hatua hiyo imejiri baada ya shambulizi la kushtukiza la kundi hilo nchini Israel mwishoni mwa wiki iliyopita.
Scholz aidha amesema kwenye hotuba yake bungeni mjini Berlin mapema leo kwamba hata mtandao wa mshikamano Palestina wa Samidoun pia utapigwa marufuku, na kusisitiza kuendelea kuiunga mkono kikamilifu Israel.
"Kwa upande wa Ujerumani kwa sasa inasimama na Israel tu. Historia yetu na wajibu wetu ulioanzia kwenye mauaji ya Wayahudi, unatufanya kuwa na jukumu lisilokoma la kusimamia uwepo na usalama wa taifa la Israel."
Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani wanalitaja kundi la Hamas linalotawala Gaza kuwa shirika la kigaidi.
Scholz aidha amelaani vikali shambulizi hilo aliloliita kuwa la kinyama na linalopingana na maadili ya Ujerumani na kusisitiza hawatakubaliana kabisa na vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi.