1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Ufaransa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

22 Januari 2020

Ujerumani na Ufaransa zimetangaza kuungana na kampuni ya uwekezaji ya BlackaRock kuongeza kasi kuvutia mtaji wa uwekezaji kwenye miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwenye nchi zinazoendelea duniani.

https://p.dw.com/p/3WdHC
Berlin | Angela Merkel und Emmanuel Macron
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Ushirikiano wa fedha na mazingira, CFP, unaijumuisha kampuni kubwa ya uwekezaji ya BlackRock, ambayo ni mmiliki mkuu wa uendeshaji wa mali na mitaji ulimwenguni, shirika la maendeleo la Ufaransa, wizara ya mazingira ya Ujerumani pamoja na idadi ya mashirika na wakfu kadhaa binafsi. Mpango huo umetangazwa leo pembezoni mwa Jukwaa la Kiuchumi Duniani linalofanyika mjini Davos, Uswisi ambako washiriki wa sekta binafsi na serikali wakiongeza shinikizo kuonesha kwamba wamedhamiria kulitatua suala la ongezeko la joto duniani.

Taarifa ya pande hizo imeeleza kuwa mpango huo unakusudia kuhamasisha uwekezaji wa mitaji ya taasisi kwenye sekta zinazohusiana na hali ya hewa kwenye masoko yanayoinukia. Uwekezaji huo unazilenga nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Amerika ya Kusini na zaidi Afrika, ambayo itapata kiasi cha asilimia 25 ya mtaji wote wa uwekezaji.

Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Nembo ya jukwaa la 50 la kiuchumi dunianiPicha: Reuters/D. Balibouse

Miradi hiyo itajumuisha nishati mbadala, nishati ya kutosha majumbani na maofisini, uhifadhi wa nishati na usafiri unaotumia umeme. Ujerumani na Ufaransa zinakusudia kuchangia Dola milioni 30 kila mmoja, huku Wakfu wa William na Flora Hewlett na wakfu wa kimazingira wa Jeremy na Hannelore Grantham zikichangia Dola milioni 10 na kujitolea Dola milioni 7.5.

Hotuba ya Trump

Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand, Helen Clark amesema hotuba ya Rais wa Marekani, Donald Trump aliyoitoa jana katika Jukwaa la Kiuchumi Duniani iliangazia zaidi masuala ya ndani ya Marekani na kuhusu kesi ya kumuondoa madarakani ambayo inamkabili.

Trump alisema anazingatia kwa umakini mkubwa kuweka vikwazo kwenye magari ya Ulaya yanayoingizwa Marekani. Aidha, amewashutumu wanamazingira aliowaita kuwa ''manabii wenye kuleta maangamizi''. Katika hotuba yake pia Trump alipinga tahadhari zinazotolewa na mwanaharakati mdogo wa mazingira Greta Thunberg.

Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Reuters/D. Balibouse

Kwa upande wake Klaus Schwab, mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wa Jukwaa la Kiuchumi Duniani, amesema katika dunia ambako wanapaswa kuwa wamoja katika utofauti, majukwaa kama hayo ya kiuchumi yanatakiwa kuendelezwa.

''Nina matumaini kwamba jukwaa hili katika siku zijazo linaweza kuwa msaada mkubwa wakati tunaposhughulikia masuala yote ambayo yanahitajika. Sisi ni sehemu ya jumuia ya kimataifa yenye mtazamo sawa. Hivyo tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vinakuwa na dunia bora zaidi kuliko dunia tuliyoirithi,'' alifafanua Schwab.

Ama kwa upande mwingine viongozi na matajiri duniani akiwemo Trump wameahidi kupanda miti ili kuisaidia dunia. Katika juhudi za kupambana na ongezeko la joto duniani, viongozi hao wamesema suala la kupanda miti ni muhimu na linapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa.

Mfanyabiashara mkubwa wa Kimarekani, Marc Benioff, amesema dunia inakabiliwa na mzozo wa mabadiliko ya tabia nchi na kwamba miti ni moja ya njia bora za kukabiliana na gesi chafu ya kaboni na kukomesha athari za mabadiliko ya tabia nchi.

(AFP, AP, Reuters)