1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Serikali kuu kuongoza vita dhidi ya COVID-19

21 Aprili 2021

Bunge la Ujerumani limepitisha sheria inayoipa mamlaka zaidi serikali kuu kuanzisha vizuizi vinavyofanana katika maeneo yaliyo na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3sKqC
Deutschland Corona-Pandemie Angela Merkel spricht im Bundestag
Picha: Tobias Schwarz/AFP

Bunge la Ujerumani limepitisha sheria inayoipa mamlaka zaidi serikali kuu kuanzisha vizuizi vinavyofanana katika maeneo yaliyo na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya corona katika wakati ambapo taifa hilo linapambana na wimbi la tatu la maambukizi.  Hatua hiyo inafuatia pendekezo la serikali ya kansela Angela Merkel baada ya kushuhudiwa changamoto kadha wa kadha huko nyuma. 

Sheria hiyo inayoruhusu kuanzishwa kwa vizuizi vya dharura katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi inakusudiwa kutumika ili kuziba mapengo yaliyojitokeza awali ambapo serikali za majimbo zilikuwa na mamlaka binafsi ya kusimamia vizuizi hivyo.

Baraza la wawakilishi Bundestag, liliipigia kura 342 sheria hiyo dhidi ya kura 250 za kuipinga na wabunge 64 hawakuwepo. Baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat linatarajiwa kuiangazia sheria hiyo kesho Alhamisi. Iwapo itapitishwa na pande zote itatumika hadi mwishoni mwa mwezi Juni.

Vizuizi vikali zaidi vitarajiwe.

Deutschand Debatte über das Infektionsschutzgesetz im Bundestag
Baraza la wawakilishi Bundestag, likiwa katika mjadala wa sheria hiyo mjini BerlinPicha: Axel Schmidt/Reuters

Mapema kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo, kansela Angela Merkel alikutana na baraza la mawaziri, ambapo kiongozi wa wabunge wa chama chake cha Christian Democrat, CDU, Ralph Brinkhaus alisema ni muhimu kuchukuliwa kwa hatua hiyo kwa kuwa hali inayoshuhudiwa kwa sasa ni tete.

Alisema "Tupo katika hali ambapo sio tu vyumba vya wagonjwa mahututi vimeelemewa, bali mfumo mzima wa afya umezidiwa. Tupo katika hali ambayo watu wengi wanaumwa na watu wengi wanakufa. Na ndio maana ni muhimu kwetu kuchukua maamuzi hii leo."

Chini ya sheria hiyo mpya, serikali kuu inataraji kutangaza vizuizi kama ukomo wa muda wa kutoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri, ukomo wa watu kukutana, kufunga maeneo ya starehe na michezo na kufunga ama kuweka vizuizi vikali kwenye maduka.

Aidha sheria hiyo itaanza kutumika kwenye maeneo ambako kutakuwa na zaidi ya maambukizi 100 kwa watu 100,00 kwa wiki. Shule zitarudi kwenye masomo ya njia ya mtandao iwapo kwango cha juu cha maambukizi kitafikia 165. Kwa ujumla, kiwango cha maambukizi kwa sasa nchini Ujerumani kimefikia 160 kwa watu 100,000 hadi hii leo ingawa kuna maambukizi makubwa ya virusi vinavyojibadilisha.

Deutschland Proteste gegen Corona-Auflagen in Berlin
Baadhi ya waandamanaji wanaoipinga sheria hiyo mpya mjini Berlin walikabiliana na polisi mapema leoPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Waandamanji wapinga sheria hiyo mpya, Berlin.

Mapema leo, jeshi la polisi lililazimika kukabiliana na waandamanaji mjini Berlin kuwatawanya wakati walipoandamana kupinga kizuizi cha kufunga shughuli ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, wakati bunge lilipokuwa linaendelea kuijadili sheria hiyo.

Kansela Angela Merkel aliiandaa sheria hiyo baada ya majimbo 16 ya shirikisho kukataa kuanzisha hatua kali zaidi licha ya ongezeko la visa maambukizi. Serikali yake mara kadhaa imekabiliwa na upinzani na machafuko kuhusiana na namna inavyoshughulikia kizuizi hicho cha kufunga shughuli na utoaji wa chanjo ambao unakwenda taratibu mno.

Jeshi la polisi limesema kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba wangewatawanya waandamanaji hao kwa kuwa hawakuwa wamevaa barakoa katika mkusanyiko huo wa watu wengi, lakini hawakuwaandamana kwa kuzingatia umbali wa kutoka kwa mut mmoja na mwingine. Hadi maafisa wa polisi 2,200 walikuwa tayari kukabiliana na maandamano hayo ya mjini Berlin.

Watu saba walikamatwa baada ya kuwashambulia polisi, na wengine walilazimika kutumia maji ya pilipili dhidi ya waandamanaji waliowarushia chupa na kujaribu kuvuka vizuizi vya polisi.

Wajerumani wamekuwa ni wagumu kukubaliana na hatua ambazo wanadhani zinaweza kutishia uhuru wao kutokana na historia ya taifa hilo la Kinazi na ujamaa, na maandamano dhidi ya sheria hiyo yamekuwa yakifanyika kwa wiki kadhaa zilizopita katika miji mbalimbali kote nchini humo.

Soma Zaidi:Ujerumani kuweka sheria ya kitaifa kudhibiti COVID-19 

Mashirika: APE