1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Ujerumani: Huenda shambulizi la Israel huko Rafah ni "kosa"

27 Mei 2024

Serikali ya Ujerumani imesema shambulizi la angani lililofanywa na Israel karibu na eneo la Rafah na kusababisha vifo vya Wapalestina 35 huenda lilikuwa ni "kosa."

https://p.dw.com/p/4gLQ7
Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Hebestreit
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit akiwa katika mnoja ya mikutano na waandishi wa habari mjini BerlinPicha: Abdulhamid Hosbas/AA/picture alliance

Ujerumani imesema hayo huku kwa mara nyingine, "ikitetea haki ya Israel ya kujilinda ndani ya msingi wa sheria ya kimataifa."

Alipoulizwa kuhusiana na madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya Israel huko Gaza, msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesema Ujerumani bila shaka italaani endapo kutatolewa ushahidi wa uhalifu kama huo.

Wakati huo huo, mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel yamechukua mwelekeo mwingine katika mkesha wa Palestina kutambuliwa kama taifa na wanachama wa umoja huo Ireland na Uhispania.

Madrid imependekeza vikwazo dhidi ya Israel kutokana na hatua yake ya kuendelea kuushambulia mji wa Rafah ulio kusini mwa Gaza.

Naye mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ambaye ni raia wa Uhispania, ameiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya ICC ambaye mwendesha mashtaka wake anataka waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahuu na wengine, wakiwemo viongozi wa Hamas.