Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kupambana na ugaidi Mali
21 Agosti 2020Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer, amesema mapambano dhidi ya ugaidi bado ni muhimu kwa sababu ugaidi bado ni tishio kubwa. Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani alitoa kauli hiyo katika eneo la kusini mwa Ujerumani la Dilligen, ambako alikuwa mwenyeji katika mazungumzo kati yake na mawaziri wenzake wa Uingereza na Ufaransa.
Mawaziri hao watatu wamewataka wanajeshi waliofanya uasi huko nchini mali kutekeleza yale waliyoahidi haraka iwezekanavyo ikiwemo kuirudisha nchi kwenye hali inayofuata katiba.
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace pia amesisitiza juu ya kurudishwa hali ya utulivu nchini Mali.
Wallace ameyataka makundi yenye silaha nchini Mali na kwenye nchi nyingine zilizo katika ukanda wa Sahel ambapo mengine yanafungamana na makundi ya Al Qaida na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS yarejee kwenye mchakato wa amani.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Florence Parly alisema kuwa wataendeleza mapambano dhidi ya ugaidi huko Mali na kuongeza kuwa hii si changamoto ya usalama katika ukanda wa Sahel tu bali pia kwa bara la Ulaya.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly pia ameeleza kwamba vikosi vya Ufaransa na vya mali vitaendelea kushirikiana katika kupambana na ugaidi licha ya kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini mali mapema wiki hii.
"Ufaransa inajihusisha na Mali kwa sababu wamali wenyewe wanataja hivyo pamoja na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vikosi vya Ufaransa havipo nchini Mali kuingilia uhuru wa Mali au wa watu wake bali vikosi vya Ufaransa vipo nchini humo kupambana na ugaidi kwa ajili ya kulinda usalama wa kila mmoja. Kwa hivyo operesheni za kijeshi zitaendelea hata bila ya kuungwa mkono na nchi zingine za Ulaya na washirika wetu wengine," alisema Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Parly.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kundi la wanajeshi waasi, wajumbe wa jumuiya ya uchumi wa nchi za Afrika magharibi ECOWAS wanatarajia kukutana hapo kesho Jumamosi nchini Mali ili kujadili juu ya mapinduzi hayo ya kijeshi.
ECOWAS imesema ujumbe huo utakaokwenda mjini Bamako utaongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan.
Vyanzo:/AFP/DPA