1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaadhimisha Siku ya Muungano

Josephat Nyiro Charo3 Oktoba 2014

Miongoni mwa wageni wapatao 800 walioalikwa kwa ibada ya ufunguzi leo (03.10.2014) katika kanisa la Marktkirche mjini Hannover ni rais wa shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck na kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/1DPOc
Tag der Deutschen Einheit 2014 Hannover
Kansela wa Angela Merkel (kushoto) na rais Joachim GauckPicha: picture-alliance/dpa/O. Spata

Maadhimisho ya siku ya Muungano wa Ujerumani yameanza leo kwa ibada katika kanisa la Kiinjili mjini Hannover. Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi ziliungana mnamo Oktoba 3 mwaka 1990.

Katika mahubiri yake wakati wa ibada ya kuyafungua maadhimisho ya Muungano wa Ujerumani leo, askofu wa kanisa la Kiinjili la Kiluteri mjini Hannover, Ralf Meister, amesema watu wote ulimwenguni wanatakiwa kukaa pamoja kama familia. Ametoa mwito kufanyike juhudi za makusudi na hatua za kujitolea kwa dhati kabisa zichukuliwe kutafuta haki. Na juhudi hizi zifanyike pia katika mizozo ya Syria na Iraq, huku akizungumzia mateso, mauaji na watu kufukuzwa makwao.

Askofu huyo amegusia kuhusu hali ngumu inayowakabili wakimbizi kaskazini mwa Iraq na Syria akisema jamii za kidini zina jukumu kubwa kusaidia kuyatafutia ufumbuzi matatizo haya kwa kupendekeza sera bora na kuanzisha midahalo watu watafakari kwa pamoja.

Huku ikiwa ni miaka 24 tangu Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi zilipoungana, na miaka 25 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin, askofu Meister ameongeza kusema dini au asili ya mtu haipaswi kutumiwa kuamua maelewano na maingiliano katika jamii.

Ralf Meister
Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Hannover.Picha: Privat

Akizungumzia muungano wa Ujerumani, askofu Meister amesema, "Muungano una maana kubwa na pana. Sio tu muundo na mpangilio. Yeyote anayezungumzia muungano, anazungumzia pia haki za kimsingi. Anayezungumzia muungano lakini kuzikataa haki msingi, katika hali halisi anafikiria maovu."

Wayahudi na Waislamu washiriki ibada

Kwa mara ya kwanza wajumbe wa Wayahudi na Waislamu wamehutubia katika ibada ya kanisani kuadhimisha siku ya muungano wa Ujerumani na wote wametoa miito ya kudumisha amani ulimwenguni. Mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha waislamu katika jimbo la Lower Saxony, Avni Altiner, amelaani vikali vitendo vinavyofanywa na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu na kusisitiza kwamba vitendo vyao ni kinyume na dini yake.

Kabla ya ibada hiyo kuanza kansela Merkel na rais Gauck walipeana mikono huku kwaya ya watoto wadogo ikiimba nyimbo zilizowaliwaza na kuwakumbusha kuhusu siku Ujerumani ilipoungana. Viongozi wengine mashuhuri waliohudhuria ibada hiyo ni spika wa bunge la Ujerumani, Nobert Lammert, rais wa zamani, Christian Wulff, kansela wa zamani, Gerhard Schröder na mawaziri wakuu kadhaa wa majimbo mengine ya Ujerumani.

Tayari hapo jana jioni mambo yalianza kupamba moto wakati sherehe za barabarani zilipofanyika. Takriban wageni 500,000 wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.

Mwandishi: Josephat Charo/DPA/EPD

Mhariri: Saumu Yusuf