Ujerumani yaandaa mkutano kuhusu Uislamu
28 Novemba 2018Mhafidhina Horst seehofer, mwanasiasa mwenye msimamo mkali, alisababisha mvutano mwezi Machi alipomkosoa moja kwa moja Kansela Angela Merkel akiipinga kauli yake kwamba "Uislamu una nafasi yake Ujerumani." Waziri mkuu huyo wa zamani wa mkoa wa Bavaria alisema Waislamu wanaoishi hapa bila ya shaka ni sehemu ya Ujerumani, lakini haimaanishi kwamba Wajerumani asilia wanaacha utamaduni na mila zao kwa kile alichokiita zingatio lisilo na ukweli, alisisitiza Seehofer wakati wa mahojiano na gazeti la Bild.
Katika mkutano wa mwaka huu kuhusu Uislamu Ujerumani, Seehofer amefanya mabadiliko, akiwaalika wanazuoni wa elimu ya dini wenye msimamo wa wastani pamoja na wanasayansi, mbali na Jumuiya za Kiislamu nchini Ujerumani. Mkutano huo unawakusanya pamoja waislamu wa Ujerumani na wawakilishi wa serikali ya Shirikisho , mikoa na serikali za mitaa. Mwaka huu Seehofer anatarajiwa kulizingatia suala la ushawishi wa kigeni kwa misikiti na jamii ya Waislamu nchini Ujerumani na hasa ushawishi wa Uturuki.
Mkono wa Uturuki katika Uislamu nchini Ujerumani
Chama cha Waislamu kwa ajili ya taasisi ya dini cha waturuki DITIB ambayo ni Jumuiya kubwa kabisa ya Kiislamu nchini Ujerumani, kinadhibitiwa na Uturuki kupitia Idara ya masuala ya dini (Diyanet) mjini Ankara, ambayo huwalipa mishahara maimamu wa kiasi ya misikiti 900 nchini Ujerumani. Jumuiya ya DITIB inakosolewa kwa kuwa karibu na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ambaye wapinzani wake wa nje na ndani wanamuangalia kama anayeiongoza nchi yake kiimla.
Kabla ya mkutano huo mjini Berlin, Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani limetoa wito kutaka paweko na imani na shughuli zinazofanywa na misikiti. Katika mahojiano na kundi la wachapishaji linalojiita mtandao wa wahariri, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani, Aiman Mazyek, alionya dhidi ya kuichukulia misikiti kuwa tatizo, akiongeza kwamba kinyume chake misikiti ni suluhisho. pamoja na hayo aliungama kwamba kuna mapungufu katika jamii za Waislamu.
Chama cha upinzani cha Kijani "Die Grüne" kimeelezea wasiwasi wake juu ya Waziriv wa ndani seehiofer kuwa mwenyekiti wa mkutano huo, huko Kiongoziv wa wabunge wa chama hicho katika bunge la shirikisho Bundestag Katrin Goering-eckard akiliambia Shirika la habari la Ujerumani DPA, kwamba muda mwingi unaotumiwa kwa mjadala, ungepaswa kwanza kutumika katika kuweka mazingira bora, badala ya kusababisha matatizo.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohamed Khelef