1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaangazia macho yake katika kombe la euro 2012

3 Januari 2012

Kocha Joachim Loew anahisi hamu ya kushinda taji akiwa na timu yake huku Ujerumani ikijitosa katika kivumbi cha ubingwa wa ulaya ikiwa na matumaini makubwa ya kunyanyua kombe lao la kwanza kuu katika miaka 16.

https://p.dw.com/p/13dMY
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim LöwPicha: picture alliance/dpa

Loew alisema nia yao ni kucheza soka ya kuburudisha na kusisimua na kasha kuandikisha ushindi katika dimba hilo, litakaloandaliwa nchini Poland na Ukraine kati ya tarehe nane Juni na Julai mosi. Ujerumani haijawahi kutwaa taji tangu mwaka 1996 lakini timu hiyo imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Tangu Loew alipochukua uongozi mwaka 2006, Ujerumani ilifika fainali ya euro 2008 na nusu fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 na kushindwa na mabingwa Uhispania katika mechi hizo zote. Hata hivyo kuimarika kwa timu ya ujerumani yenye wachezaji chipukizi kama vile mesut oezil imewapa hesima kubwa kutoka kwa mahasimu wao.

Loew anasema ijapokuwa ujerumani inaonekana kuwa timu bora katika kinyanganyiro hicho, kunazo timu tano zinazimnyima usingizi. Nazo ni Uholanzi, Ureno, Ufaransa, Uingereza na Italia. Ujerumani iko katika kundi moja na uholanzi, ureno pamoja na Denmark lakini Loew anasisitiza kuwa hamwogopi yeyote na badala yake anatarajiwa kuwa na mechi za kuvutia.

Kwingineko Mchezaji wa klabu ya Bayern Munich Bastian Schweinsteiger amefichua kuwa anasifiwa kwa kulinganishwa na wachezaji Xavi na Andres Iniesta, lakini anaamini kuwa yeye ni mchezaji tofauti ikilinganishwa na nyota hao wawili wa Barcelona. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anayechezea timu ya taifa ya ujerumani kwa mara nyingi amelinganishwa na wahispania hao wawili na kocha wa klabu yake ya Bayern Jupp Heynkes ambaye alichukua hatamu za uongozi katika uga wa Allianz Arena msimu uliopita. Schweinstiger alisema kweli Xavi na Iniesta ni viungo mahiri ijapokuwa yeye anajiona kuwa tofauti kidogo. Kwa sababu ana uwezo wa kupata mipira ya angani katikati mwa uwanja labda kwa sababu ya maumbile na kimo chake.

Mchezaji wa Bayern Bastian Schweinsteiger akisheherekea bao lake
Mchezaji wa Bayern Bastian Schweinsteiger akisheherekea bao lakePicha: dapd

Schweinsteiger ameichezea Bayern zaidi ya mara 350 tangu alipojiunga nayo mwaka 2002 pia amemsifu kocha wake Heynckes kwa kuifufua timu hiyo. Miamba hao walimaliza wa tatu msimu uliopita katika ligi ya Bundesliga, alama kumi nyuma ya mabingwa watetezi Borussia Dortmund, lakini baada ya kumaliza mwaka wa 2012 kwa ushindi mara tatu mfululizo, kwa sasa wanaongoza jefwali alama tatu mbele ya Dortmund na Schalke. Mjerumani huyo anasema kombe la ligi ya mabingwa ndilo lengo lao kuu msimu huu. Schweinsteiger amehusishwa na uvumi wa uhamisho wa vilabu kadhaa vikuu barani ulaya ikiwemo Manchester United Real Madrid na hasa AC Milan. Lakini Bayern imesisitiza kwua nyota wao huyo haendi kokote. Wakati huo huo klabu hiyo ya Bayern Munich iko katika kambi ya mazoezi nchini Qatar.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Yusuf Saumu