Ujerumani yaionya NATO kuhusu kuimarika kwa China kijeshi
3 Desemba 2020Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema Muungano wa Kujihami wa NATO katika harakati za kutaka kuufanyia mabadiliko muungano huo, miongoni mwa mambo wanayostahili kuyafikiria ni kuhusu kuebuka kwa China kama Mojawapo ya nchi zenye nguvu kubwa za kijeshi duniani.
Matamshi haya ya Maas yamekuja baada ya siku mbili za mkutano uliowakutanisha mawaziri wa mambo ya nje wa muungano huo wa NATO wenye nchi 30 wanachama.
Maas amesema ni lazima wabuni njia iliyofikiriwa vyema kuhusiana na China na kwamba kutakuwa na nafasi watakazoweza kuzitumia na vile vile changamoto wanazostahili kujiandaa kukabiliana nazo. Kuhusiana na Afghanistan na mpango wa NATO wa tangu 2014, Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema lengo ni kuwahakikishia Waafghanistan kwamba wanapata haki zao.
"Sisi kama wanachama wa NATO tunataka kuhakikisha kwamba vikosi zaidi vya majeshi Afghanistan vinapunguzwa kwa masharti yaliyo wazi. Afghanistan inahitaji usalama na uhuru. Haki za raia zilizopatikana kwa juhudi kubwa katika miaka ya hivi karibuni ni lazima zilindwe.” alisema Maas
Amesema pia anatarajia kuwa wanajeshi wa Marekani wataendelea kuwaunga mkono wanajeshi wengine katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati iliyozongwa na machafuko. Rais wa Marekani Donald Trump ana mpango wa Kupunguza nusu ya wanajeshi wa Marekani Afghanistan ili wasalie wanajeshi 2,500 tu nchini humo. Ila kuna matumaini miongoni mwa wakosoaji wa mpango huo kwamba rais mteule wa Marekani Joe Biden huenda akabadilisha msimamo wa Marekani kuhusiana na suala hilo.
Huku mazungumzo ya amani na kundi la Taliban yakiwa yanaendelea, NATO yenyewe inatafakari kuhusiana na mpango wake wa kijeshi Afghanistan. Kulingana na Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, uamuzi huu mgumu utafanywa katika kikao cha mawaziri wa ulinzi kitakachofanzika mwezi Februari. Stoltenberg ameonya mara kadhaa kuhusiana na kuwaondoa wanajeshi kwa haraka na kuhatarisha usalama uliopatikana nchini humo.
Heiko Maas lakini amesema wanajeshi wa Ujerumani, Bundeswehr, hawatokuwa Afghanistan milele. Ila kabla yote hayo jukumu la kwanza la NATO ni kuhakikisha kwamba inasitisha mizozo baina ya nchi wanachama. Maas amesisitiza bila kuzitaja Uturuki na Greece ambazo zimekuwa zikizozana kuhusiana na Cyprus na madini yaliyoko baharini, kwamba mizozo baina ya wanachama ni hatari kwa muungano huo.