Ujerumani yaishutumu Marekani kwa vikwazo vya mradi wa gesi
21 Desemba 2019Urusi na Umoja wa Ulaya pia zimetoa taarifa zinazokosoa vikwazo hivyo, siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutia saini kuwa sheria hatua ya kuzuwia mali na upatikanaji wa visa kwa wale wanaohusika katika mradi huo wa Nord Stream 2.
Wabunge wa Marekani wanataka kuzuwia kile wanachokiona kuwa ni ongezeko la utegemezi wa nishati kutoka Urusi katika mataifa ya Ulaya magharibi kwa kulenga mradi huo, ambao una lengo la kuongeza maradufu usambazaji wa gesi asilia kutoka Urusi nchini Ujerumani kupitia katika bomba lililowekwa chini ya bahari ya Baltiki.
Vikwazo hivyo vinalenga wakandarasi wanaofanyakazi katika kutandika bomba hilo la Nord Stream 2, mradi wenye thamani ya euro bilioni 10 unaotarajiwa kukamilika mapema mwaka 2020, na mradi mwingine wa gesi wa Urusi , unaojulikana kama TurkStream.
Katika ishara ya kwanza kwamba vikwazo hivyo vinaanza kuuma, mkandarasi kutoka Uswisi Allseas imesitisha shughuli zake katika mradi huo wa Nord Stream 2 wakati ikisubiri maelezo kutoka maafisa wa Marekani kuhusiana na vipengee vya hatua hizo.
Licha ya kuwa bunge la Marekani waliunga mkono kwa kiasi kikubwa vikwazo, kulikuwa na baadhi wamekosoa hatua hiyo ambayo kimsingi inawaadhibu washirika wa NATO kama Ujerumani.
Wakati msemaji wa Umoja wa Ulaya amekosoa kile alichokiita "uwekaji wa vikwazo dhidi ya makampuni ya Umoja wa Ulaya yanayofanyakazi halali", serikali ya Ujerumani imesema Berlin inakataa "aina hii ya vikwazo dhidi ya mataifa ya kanda".
Athari kwa makapuni ya Ulaya
"Hatua hii itayaathiri makampuni ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya na kufikia katika uingiliaji wa masuala yetu ya ndani," amesema msemaji wa kansela Angela Merkel , Ulrike Demmer.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi Maria Zakharova ameishutumu Marekani kwa kuendeleza nadharia ambazo zinazuwia biashara ya dunia, na kuongeza katika ukurasa wake wa Facebook: "Hivi karibuni watadai kuwa tuache kupumua."
Lakini Marekani sio taifa pekee kuhoji kuhusu mradi huo, Ukraine , Poland na baadhi ya mataifa ya eneo la Baltiki pia yameeleza shaka yao.
Ukraine imekuwa na wasi wasi kuwa bomba hilo jipya litaiondoa katika biashara ya gesi na kuruhusu urusi kuongeza mbinyo kuhusiana na masuala mengine.
Wabunge wa Marekani wameeleza kuiunga mkono Ukraine kama sehemu ya hatua yake hiyo ya kisheria ya kuweka vikwazo.
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imesema jana Jumamosi kwamba inachunguza athari za vikwazo vya Marekani dhidi ya makampuni ya Umoja wa Ulaya yanayohusika katika ujenzi wa bomba la Nord Stream 2 chini ya bahari ya Baltiki.
Kama suala la msingi, Umoja wa Ulaya unapinga uwekaji wa vikwazo dhidi ya makampuni ya Umoja huo yanayofanya kazi halali," amesema msemaji wa halmashauri hiyo.