Ujerumani yataka Ugiriki ibakie katika kanda ya Euro
5 Januari 2015Gabriel, waziri wa uchumi wa Ujerumani na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD, pia ameliambia gazeti la Hannoversche Allgemeine kwamba kanda ya euro imeimarika katika miaka ya hivi karibuni na haiwezi kutishwa. Katika mahojiano na gazeti hilo yaliyochapishwa hivi leo waziri huyo ameongeza kusema, "Lengo la serikali ya Ujerumani, Umoja wa Ulaya na hata serikali ya Athens ni kuhakikisha Ugiriki inabakia katika kanda inayotumia sarafu ya euro."
Gabriel amesema wanatarajia serikali ya Ugiriki kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na Umoja wa Ulaya, bila kujali atakayeiongoza, akizungumzia uchaguzi wa Ugiriki uliopangwa kufanyika Januari 25 na uwezekano wa mabadiliko ya serikali mjini Athens.
Ralph Brinkhaus, mbunge wa chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, amesema ana matumaini serikali mpya ya Ugiriki itaendelea kuiongoza nchi hiyo katika mkondo wa Umoja wa Ulaya. "Hakuna anayetaka Ugiriki itoke kanda ya euro kwa kuwa itagharimu fedha nyingi na lazima isisitizwe kwamba hatua hiyo itafuta miaka minne ya sera ya mageuzi ya nchi hiyo. Ndio maana tuna matumaini uchaguzi wa bunge utaleta matokeo yatakayoendelea kuifanya Ugiriki iegemee Ulaya."
Awali Georg Streiter, msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema serikali ya Ujerumani inatarajia Ugiriki itaheshimu masharti ya makubaliano ya mpango wa uokozi wa thamani ya euro bilioni 240 kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF.
Streiter alisita kutoa kauli kuhusu ripoti ya jarida la Der Spiegel toleo la Jumamosi kwamba serikali ya mjini Berlin imebadili mtizamo wake na sasa inaamini kanda ya euro itaweza kumudu iwapo Ugiriki itajiondoa kutoka kwa kanda ya euro, kama ikihitajika.
Kanda ya euro kuhimili kujiondoa kwa Ugiriki
Jarida hilo limeripoti kuwa serikali ya Ujerumani inachukulia kutoka kwa Ugiriki kutoka kwenye kanda hiyo kuwa jambo lisiloweza kuepukika kama chama cha siasa za mrengo wa shoto cha Syriza, kinachoongoza kwa asilimia ndogo katika kura za maoni, kitashinda uchaguzi ujao wa Ugiriki. Chama hicho kinataka kufuta hatua za kubana matumizi na sehemu kubwa ya deni la Ugiriki.
Jarida hilo limeripoti kuwa kansela Merkel na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble sasa wanaamini kanda ya euro imetekeleza mageuzi ya kutosha tangu kilele cha mzozo wa madeni mwaka 2012 kuweza kukabiliana na uwezekano wa Ugiriki kujitoa kutoka kwa kanda hiyo.
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeiona ripoti ya Der Spiegel kama juhudi za Merkel na Schäuble kuwashinikiza Wagiriki na kiongozi wa chama cha Syriza, Alexis Tsipras. Ofisi za Merkel na Schauble hazikuthibitisha wala kukanusha ripoti hiyo iliyokosolewa vikali na wanachama wa vyama vya CDU na SPD na kumuweka kansela Merkel katika shinikizo kutoka kwa vyama vidogo washirika katika serikali yake.
Peter Bofinger, mmoja wa wazee wa busara wa baraza la washauri wa kiuchumi kwa serikali ya Ujerumani ameonya dhidi ya kujitoa kwa Ugiriki kutoka kwa eneo la euro akisema hatua hiyo itasababisha kitisho kikubwa kwa uthabiti wa kanda hiyo.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba