Ujerumani yawataka wahamiaji kurejea makwao kwa hiari
3 Desemba 2017Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere ameliambia gazeti la Bild am Sonntag kwamba mpango huo ni kwa ajili ya kuwasaidia kutengamana tena pindi watakaporejea nchini mwao. Kwa miaka kadhaa Ujerumani imekuwa ikitoa msaada wa fedha kwa wahamiaji wote waliokataliwa kupewa hifadhi, ili kuwasaidia waweze kurejea kwenye nchi zao, zikiwemo gharama zinazohusiana na safari pamoja na fedha za kuanzia maisha pindi watakaporejea.
De Maiziere amesema juu ya hilo, familia zinaweza kupatiwa hadi Euro 3,000 na mtu mmoja mmoja akipatiwa hadi Euro 1,000 kama wataamua kurejea nyumbani kwa hiari ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari. ''Ukiamua kurejea nyumbani kwa hiari ifikapo wakati huo, ili kukusaidia kuanza maisha mapya, unaweza ukapewa fedha za kugharamia makaazi kwa mwaka mmoja ukiwa kwenye nchi yako,'' amesema de Maiziere.
Fedha kwa ajili ya nyumba
Kwa mujibu wa gazeti la Bild am Sonntag, mbali na malipo ya awali watakayopewa watu ambao maombi yao ya hifadhi yamekataliwa, pia wanaweza kupewa fedha kwa ajili ya kulipia kodi ya nyumba wakiwa nchini mwao, kujenga nyumba, kukarabati nyumba au hata kununua vitu muhimu kwa ajili ya jikoni ua bafuni. De Maiziere amesema mpango huo utaitwa ''Nchi yako. Mustakabali wako. Ni sasa!'' Amesema kuna fursa nyingi katika nchi zao.
Shirika la Ujerumani linalohusika na kuwasaidia wakimbizi, Pro Asyl, limeukosoa mpango huo, likisema ni mkakati usio na manufaa na sio wa kuaminika. Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Guenter Burkhardt, ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba serikali inajaribu kuwashawishi watu kuacha kuzitetea haki zao bila ya kupata msaada makini.
Mpango huo wa de Maiziere umetolewa wakati ambapo jimbo la Bavaria ambalo linawarudisha raia wengi kutoka Afghanistan kuliko jimbo lolote lile la Ujerumani, limeripoti kuhusu matatizo ya kuwatafuta watu ambao wanatakiwa kurejeshwa makwao.
Wizara ya mambo ya ndani ya jimbo la Bavaria, imeliambia gazeti la Welt am Sonntag kwamba Waafghanistan wengi ambao waligundua kwamba wanakaribia kurejeshwa makwao, mara nyingi wanatoroka siku chache kabla ya kuondoka kwa ndege zao. Kwa mujibu wa wizara hiyo, ilishuku kwamba watu wengi waliokuwa wanatakiwa kurejeshwa makwao, wengi wao ambao walikuwa wahalifu, walikuwa wakisaidiwa kutoroka na mashirika ya Ujerumani yanayowasaidia wakimbizi.
Pendekezo la Wasyria kurudishwa lapingwa
Wakati huo huo, mipango ya hivi karibuni ya mawaziri wa mambo ya ndani kutoka vyama vya Christian Democratic Unioni, CDU na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU ya kuanza tena kuwarudisha makwao Wasyria ifikapo katikati ya mwaka 2018, imepingwa na viongozi wengine wa CDU.
Mkuu wa kundi la wabunge wa vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU na CSU, Volker Kauder, ameliambia gazeti la Welt am Sonntag kwamba hatua kama hiyo ya kuwarejesha nyumbani Wasyria kwa sasa sio muhimu kwake, kwa kuzingatia hali ya usalama. Hata hivyo, amesema hali hiyo inabidi iangaliwe upya mara kwa mara.
Pendekezo la kuwarejesha nyumbani wahamiaji, ambalo limewasilishwa na majimbo ya Bavaria na Saxony limeidhinishwa kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani, utakaofanyika wiki ijayo mjini Leipzig.
Pendekezo hilo limekosolewa vikali na wanasiasa wa chama cha Social Democratic, SPD, chama kinacholinda mazingira cha Kijani na chama kinachofuata siasa za mrengo wa kushoto, Die Linke. Pendekezo hilo litawaathiri zaidi wahalifu na wahamiaji ambao maombi yao ya kupewa hifadhi yamekataliwa.
Mwandishi: Grace Kabogo/DPA, AP, Bild am Sonntag, http://bit.ly/1KgGZCp
Mhariri: Caro Robi