Ujumbe wa IAEA kukizuru kinu cha nyuklia cha Zaphorizhizhia
29 Agosti 2022Grossi ambaye anauongoza ujumbe huo amesema Jumatatu kuwa watafika katika kinu hicho kikubwa kabisa cha nyuklia barani Ulaya baadae wiki hii. Hata hivyo, Grossi hakufafanua zaidi kuhusu siku ambayo ujumbe huo utawasili. Kinu hicho kilichoko Ukraine, kinadhibitiwa na jeshi la Urusi na kimekuwa kikilengwa kwa mashambulizi katika wiki za hivi karibuni. Urusi na Ukraine zimekuwa zikitupiana lawama za mashambulizi ya makombora yanayofanywa karibu na kinu hicho, jambo linalozusha hofu ya kutokea maafa ya mionzi.
Katika ukurasa wake wa Twitter, Grossi ameandika kuwa lazima usalama uhakikishwe katika kinu hicho cha nyuklia. IAEA imesema ujumbe wake utatathmini mazingira ambayo wafanyakazi wanaendesha shughuli zao katika kiwanda hicho, uharibifu, pamoja na kukagua mifumo ya usalama. Pia utafanya shughuli za ulinzi wa dharura kuangalia jinsi nyenzo za nyuklia zinavyofanya kazi.
Urusi yaukaribisha ujumbe wa IAEA
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Urusi amesema Jumatatu kuwa nchi yake inaukaribisha ujumbe huo wa IAEA kukizuru kinu cha nyuklia cha Zaporizhizhia. Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa kudumu wa Urusi katika mashirika ya kimataifa yaliyoko mjini Vienna, amesema Urusi imechangia kwa kiasi kikubwa katika ziara hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba ameonya kuwa ujumbe wa IAEA katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia utakuwa mgumu zaidi katika historia ya shirika hilo. Kuleba ameyasema hayo kwa kuzingatia mapigano yanayofanywa na majeshi ya Shirikisho la Urusi, huku nchi hiyo ikiendelea kujaribu kuhalalisha uwepo wake.
Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema kuwazuia kabisa raia wa Urusi kuingia kwenye nchi wanachama za umoja huo sio wazo zuri, huku kukiwa na ripoti kuwa nchi hizo zilikuwa zinajiandaa kusitisha makubaliano ya visa na Urusi.
''Sidhani kama kufuta kabisa uhusiano na raia wa Urusi kutasaidia. Na sidhani kama wazo hili litakuwa na umoja unaohitajika. Nadhani tunapaswa kuangalia jinsi Warusi wengine wanavyopata visa. Lakini sikubaliani na kuacha kabisa kutoa visa kwa Warusi wote,'' alisisitiza Borrell.
Baadae wiki hii, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watajadili ombi linaloongozwa na Ukraine la kuwapiga marufuku watalii wa Urusi kuizuru Ulaya. Wazo hilo litakalojadiliwa katika mkutano wa siku mbili utakaofanyika kuanzia Jumanne mjini Prague, limezigawa nchi za Umoja wa Ulaya, huku baadhi yao wakikubaliana nalo na wengine wakipinga, wakihofia kuwa litafunga milango kwa wapinzani wa Urusi wanaotaka kuikimbia nchi yao.
ICRC kutathmini shughuli za kiutu
Ama kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu, ICRC, Robert Mardini anaelekea nchini Ukraine wiki hii kwa ajili ya kuangalia shughuli za kibinaadamu pamoja na kukutana na jamii zinazopewa msaada wa kiutu.
Nayo Idara ya Ujasusi ya Urusi, FSB imesema imemgundua raia wa pili wa Ukraine anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya Daria Dugina, binti wa mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladmir Putin, ambaye ana misimamo mikali na anatetea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Alexander Dugin.
Huku hayo yakijiri wizara ya ulinzi ya Urusi imesema Jumatatu kwamba Urusi inapanga kufanya luteka kubwa ya kijeshi itakayowahusisha zaidi ya wanajeshi 50,000, silaha 5,000 na vifaa kadhaa vya kijeshi, ndege 140 za kivita pamoja na meli 60 za kivita.
(DPA, AFP, AP, Reuters)