1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Umoja wa Afrika umeanza mazungumzo nchini Libya

Abdu Said Mtullya11 Aprili 2011

Kanali Gaddafi aukubali mpango wa amani uliowasilishwa na ujumbe wa Umoja wa Afrika,

https://p.dw.com/p/10r7Y
Kiongozi wa Libya Kanali GaddafiPicha: AP

Ujumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika wakiwemo marais wanne, umeanza juhudi za kusuluhisha nchini Libya.

Baada ya kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kanali Gaddafi mjini Tripoli , Rais Zuma wa Afrika Kusini amesema kuwa serikali ya Libya imeukubali mpango wa amani uliowasilishwa na Umoja wa Afrika.

Ujumbe huo sasa unatarajiwa kukutana na wawakilishi wa wapinzani katika mji wa Benghazi.Hapo awali ujumbe wa Umoja wa Afrika ulisisitiza ulazima wa kusimamisha mapigano yote na kuanzisha kipindi cha mpito ili kuelekea kwenye mageuzi. Lakini msemaji wa wapinzani ameeleza kuwa mapigano asilani hayatasimamishwa ikiwa Gaddafi hatajiuzulu kwanza.

Ujumbe wa Umoja wa Afrika umewasili nchini Libya huku ndege za jumuiya ya kijeshi ya NATO zikifanya mashambulio na kuviteketeza vifaru 25 vya majeshi ya Gaddafi.

Wakati huo huo mapigano makali yameendelea katika miji ya Adjabiya na Misrata.Na kamanda wa waasi ameeleza kuwa mashambulio yaliyofanywa na ndege za NATO yalisaidia kuyazuia majeshi ya Gaddafi kusonga mbele katika mji wa Adjabiya.

Waliokuwamo katika Ujumbe wa nchi za Umoja wa Afrika ni pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini,Marais wa Mali,Congo,Mauritania na waziri wa mambo ya nje wa Uganda. Wajumbe hao walilakiwa na wafuasi wa Gaddafi waliokuwa na picha za kiongozi wao na bendera za rangi ya kijani za utawala wake.