Ukame waathiri utalii Afrika Kusini
6 Januari 2020Maeneo kadhaa ya nchi hiyo yameathiriwa pakubwa kufuatia miaka mfululizo ya hali ya hewa isiyo ya kawaida na mvua za chini ya kiwango ambazo zimesababisha ukame na kukauka kwa vyanzo vya maji tangu mwaka 2015, ambao unatajwa kuwa mwaka uliovunja rekodi ya ukame nchini humo katika historia.
Mamlaka inayosimamia hifadhi za taifa ya nchini Afrika Kusini, WRSA inakadiria kwamba jimbo la Cape Kaskazini limepoteza zaidi ya theluthi mbili ya wanyama kwenye hifadhi zake katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Mamlaka hiyo inaendesha utafiti wa kitaifa kuangazia kiwango cha wanyama waliokufa pamoja na athari za kifedha kwenye zaidi ya ranchi 9,000 kote nchini humo.
Mkuu wa WRSA Adri Kitshoff-Botha amenukuliwa akisema huo ni ukame usio wa kawaida, si ukame wa mwaka mmoja ama miwili, kwani kuna baadhi ya maeneo ambako kumeshuhudiwa ukame ukiendelea hadi miaka sita".
Sekta ya wanyama pori inachangia pakubwa kwenye pato litokanalo na eneo zima la utalii, uwindaji na uzalishaji wa nyama. Uwindaji unaofanywa kama mchezo wa kuwania tuzo, pekee ulichangia randi bilioni mbili ama Dola milioni 140 mwaka 2016, hii ikiwa ni kulingana na utafiti uliofanywa kwa ajili ya wizara ya mazingira.
Kulingana na jopo la Kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kiwango cha joto nchini humo kinapanda mara mbili ya wastani wa kawaida wa dunia, na kitisho sasa kikiwa ni kupungua kwa maji kwenye vyanzo na hifadhi zake.
Meneja wa hifadhi ya Thuru Lodge iliyoko jimbo hilo la Cape Kaskazini, Burger Schoeman, amesema athari ya ukame kwenye uoto na ardhi kavu vimeendelea kutishia pakubwa sekta hiyo.
Hifadhi hiyo ambayo awali ilikuwa na wanyama pori wapatao 4,500, ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za spishi kuanzia mijusi hadi faru, hivi sasa hifadhi hiyo imepoteza karibu wanyaman 1,000 kutokana na ukame. Mizoga inaongezeka katika machimbo yaliyotelekezwa pambeni mwa hifadhi hiyo.
Schoeman amesema wako katika kipindi ambacho wanajibana sana. Fedha zote wanazopata kutokana na mauzo ya wanyama, nyama na vitu vingine, hurudishwa zote kwenye hifadhi kwa ajili ya matunzo ya wanyama waliosalia.
Hifadhi hiyo imeshuhudia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, wakati inaponunua chakula cha ziada kwa ajili ya wanyama, lakini wawindaji wanalipa pesa kidogo na watalii wachache mno wanatembelea hifadhi, huku wanyama wenyewe wakiwa na hali mbaya.
Kwenye hifadhi ya Karreekloof Safari Lodge yenye ukubwa wa hekta 48,000 ambayo pia iko kwenye jimbo hilo, walinda hifadhi hukutana na mizoga ya wanyama kila kukicha. Hakuna mtu anayetaka kununua hifadhi hizo kwa kuwa nao wanakabiliwa na changamoto kama hiyo ya ukame, amesema meneja wa hifadhi hiyo Gideon Watts na kuongeza kuwa hifadhi yake imepata robo ya mvua ya wastani wa mvua za kawaida msimu huu.
Kulingana na WRSA, sekta ya uhifadhi imeshuhudia anguko la karibu asilimia 20 ya idadi ya watalii kwa mwaka jana. Ukame pia umeathiri eneo lililobaki, huku Botswana ambako kunapatikana theluthi ya tembo wote wa Afrika, pia imeshuhudia zaidi ya tembo 100 wakifa katika miezi miwili tu mwaka jana.