Ghasia za walowezi wa Kiyahudi zazidi Ukingo wa Magharibi
14 Novemba 2023Wiki chache zilizopita zimekuwa ngumu sana, alisema Halima Khalil Abu Eid.
Mama huyo wa wasichana wawili wadogo anaishi Khirbet Susiya, kijiji kilichoko Kusini mwa Milima ya Hebron katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli.
Mwezi mmoja uliopita, wakati familia hiyo ikiwa imelala, walowezi wa Kiyahudi walivamia nyumba ya familia yake, wakampiga mumewe na kuwatishia kwa muda wa mwisho.
"Lazima muondoke mahali hapo. Msipoondoka, tutakupigeni risasi. Na lazima mvunje nyumba yanu," alisema Abu Eid, akisimulia onyo alilopokea usiku huo.
Tangu vita vya Israel na Hamas kuanza, Abu Eid alisema, walowezi wamezidisha shinikizo lao kwa wakaazi wa Khirbit Susiya. "Wanasaka, wanatuharibu na kututia hofu, na mara ya mwisho pia walimshambulia mume wangu na shemeji yake." Mmoja wa binti zake alikuwa akitapika kwa hofu, alisema.
Khirbet Susiya imeshuhudia miaka ya unyanyasaji wa walowezi wanaoishi katika makazi ya karibu na mashamba ya kilowezi. Lakini tangu Oktoba 7, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu umeshuhudia ongezeko "kubwa" la ghasia za walowezi na kufurushwa kwa Wapalestina, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA.
Soma pia: Vikosi vya Israel vyauwa Wapalestina 7 Ukingo wa Magharibi
Oktoba 7, shambulio la Hamas - linalochukuliwa kuwa shirika la kigaidi na Umoja wa Ulaya na Marekani - liliua takriban watu 1,200 wanaoishi katika jamii za kusini mwa Israeli karibu na Ukanda wa Gaza na kushudia wengine wasiopungua 239 wakichukuliwa mateka, kwa sasa wanashikiliwa mateka huko Gaza.
Shambulio hilo limesababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya anga yanayoendelea kutoka Israel na mashambulizi ya ardhini huko Gaza. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas, mashambulizi ya Israel katika eneo hilo lililozingirwa yameua zaidi ya Wapalestina 11,000 huko Gaza. Makombora bado yanarushwa kuelekea Israel.
Vurugu za walowezi katika Ukingo wa Magharibi
Vita vya Israel na Hamas vinawaathiri pia Wapalestina ambao wapo katika Ukingo wa Magharibi, kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya Kibinadamu OCHA, Wapalestina takriban 168 wameuwawa na majeshi ya Israel yanayouakalia ukingo huo wa Magharibi kimabavu, huku wengine wanane wakiuwawa na walowezi wakiyahudi. Waisraeli watatu wameuawa katika mashambulizi ya Wapalestina.
Kwa Mujibu wa Umoja wa Mataifa watu wapatao 1,149 kutoka katika jamii 15 za Wabedui na wakulima wamelazimika kuyahama makazi yao, wakilazimishwa kubomoa makaazi yao na mazizi ya mifugo. Wengine hawakuweza kuchukua mali zao. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamerekodi visa kadhaa, ambapo walowezi wenye silaha waliingia katika vijiji vya wapalestina na kuwatishia wakaazi iwapo hawataondoka.
Khirbet Susiya ni jamii ndogo ya Kipalestina iliotawanyika katika vilima, wengi wakijihusisha na kilimo pamoja na ufugaji wa wanyama kama shughuli kuu ya kiuchumi. Mmoja wa wakaazi kutoka jamii hiyo Abu Eid alisema walifahamu kitambo kwamba walowezi walitaka kupora mali zao ikiwemo nyumba, hivyo hawataondoka katika ardhi hiyo kwa sababu ndio nyumbani kwao.
Soma pia: Saudi Arabia yatuma mjumbe kwenye ukingo wa Magharibi
"Twende wapi? Wanataka nini kutoka kwetu? Wanataka tu kuchukua nyumba zetu; tunalijua hili tangu zamani. Tunaweza kwenda wapi? Hii ni nyumba yetu, hii ni nyumba yetu, hatuwezi kuiacha. ,” alisema Abu Eid.
Uharibifu wa miundombinu na unyanyasaji
Wakazi wa Khirbet Susiya hivi sasa wanalazimika kupanda kuta na vilima vilivyotengenezwa kwa udongo ambavyo vinazuia njia za kuingia, na kupita ndani ya kijiji.
"Ilikuwa Oktoba 16, walowezi waliovalia sare na askari walikuja hapa, ikiwa ni pamoja na tingatinga lililokuwa likiendeshwa na walowezi tunaowafahamu. Walifunga njia zote za kuingia Susiya, na pia kuharibu visima viwili vya maji," anasema Nasser Nawaj'ah, mtafiti wa ndani wa shirika la kutetea haki za binadamu la Israel B'Tselem, ambaye pia anaishi Khirbet Susiya. Birika jingine liliharibika na baadhi ya mabomba ya maji yalikatwa pia, alieleza Nawaj'ah.
Baadhi ya wakaazi katika eneo hilo kwa sasa wanategemea uwepo wa wanaharakati wa Israel ambao wanakuwepo kijijini hapo kwa saa 24, lakini nao wameshambuliwa katika maeneo kadhaa na walowezi ambao baadhi yao walikuwa wamevalia sare za kijeshi.
Yehuda Shaul ni mwanaharakati wa Israel na mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Israel Breaking the Silence, ambaye sasa anafanya kazi katika shirika tofauti la Ofek. Shaul kwa sasa anatumia muda wake mwingi katika Milima ya Hebron Kusini kusaidia wanakijiji.
Yehuda Shaul ni mwanaharakati wa Israel na mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Israel Breaking the Silence, ambaye sasa anafanya kazi katika shirika tofauti la Ofek, ili kusaidia wanakiji.
"Kwa miaka mingi jeshi halikuingilia kati kulinda Wapalestina, lakini tangu Oktoba 7 wakati vita vilipoanza, tuna ukweli leo ambapo timu za uitikiaji wa haraka katika makazi, hawa ni walowezi wa ndani, waliajiriwa kama askari wa akiba, na sasa wanafanya kazi wakiwa wamevalia sare wakiwa na bunduki na vifaa kamili kwa mamlaka ya wanajeshi," Shaul aliiambia DW. "Wapalestina kimsingi hawana chochote cha kuwalinda tena," aliongeza.
Soma pia: Rais wa Mamlaka ya Palestina Abbas azuru mji wa Jenin
Jeshi la Israel lilisema kwamba katika taarifa yake, "dhamira ya IDF ni kulinda usalama wa wakaazi wa eneo hilo na kuchukua hatua kuzuia ugaidi na shughuli zinazohatarisha maisha ya raia wa Israel, na chombo kikuu chenye jukumu la kushughulikia madai ya ukiukwaji wa sheria ni polisi ya Israeli.
Majibu ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) yameongeza kuwa wakiwa katika eneo hilo, wanajeshi hukutana na matukio ya vurugu yanayoelekezwa kwa Wapalestina au mali zao.
"Katika matukio hayo, askari wanatakiwa kuchukua hatua ili kukomesha ukiukwaji huo na ikibidi kuwachelewesha au kuwaweka mahabusu watuhumiwa hadi polisi wafike eneo la tukio.(...) Katika hali ambayo askari wanashindwa kufuata maagizo ya IDF, matukio hayo yanapitiwa kwa kina, na hatua za kinidhamu zinatekelezwa ipasavyo,” ilisema taarifa hiyo.
Ongezeko la mashambulizi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya Kibinadamu OCHA, zaidi ya mashambulizi 240 ya walowezi dhidi ya Wapalestina yamerekodiwa tangu Oktoba 7, Umoja wa Mataifa unasema kwamba hii inaakisi kuongezeka kwa visa. Viwango vya sasa vinaonesha kwamba visa saba kwa siku hutokea, ikilinganishwa na visa vitatu kwa siku kabla ya kuzuka kwa vita.
Mashambulizi haya yamesababisha kuhama na kuruhusiwa kwa jamii nzima, haswa katika eneo C, ambalo linaunda takriban asilimia 60 ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa. Eneo C liliundwa chini ya Makubaliano ya Oslo ya mwaka 1995 na lilikusudiwa kuhamishiwa hatua kwa hatua hadi kwenye mamlaka ya Palestina lakini bado linaendelea kuwa chini ya usalama kamili na udhibiti wa utawala wa Israel.
Rais wa Marekani Joe Biden amelaani ghasia katika eneo la Ukingo wa Magharibi kwa kusema "lazima isitishwe na wawajibishwe." Wakati waziri wa mambo ya kigeni Ujerumani Annalena Baerbock hivi karibuni alipotembelea Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan alionya kwamba "eneo hilo lisitumbukizwe kwenye vurugu."
Soma pia: Jenin: Kwanini eneo hili limekuwa chanzo cha ghasia?
Kuna haja ya dharura kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kufikia suluhu la kisiasa, anasema Shaul, mwanaharakati wa Israel. "Hutaweza kuunda taifa la Palestina kutokana na viunga 165 ambavyo vimetenganishwa na makazi na eneo C linalotawaliwa na walowezi," alisema Shaul. "Hakuna mataifa mawili bila Eneo C kwa Wapalestina."
Kwa baadhi ya Wapalestina, msaada umechelewa kufika. Salah Abu Awad ni mchungaji kutoka jamii tofauti iliyo karibu. Alilazimika kuondoka nyumbani kwake na maeneo ya malisho mnamo Oktoba 15, baada ya mashambulizi ya mara kwa mara ya walowezi na vitisho dhidi ya wanakijiji. "Walikuja kila Ijumaa na Jumamosi, wakiharibu vitu, wakitutishia. Nilichoka, nikaondoka," alisema Abu Awad.
Abu Awad alikuwa tayari amehama mara kadhaa hapo awali kwa sababu ya vitisho na manyanyaso. Katika eneo lake la sasa, hana malisho ya kondoo au mbuzi wake, na hajui atafanya nini baadaye.
"Mimi ni mchungaji. Bila kondoo wangu, mimi si kitu. Ninapaswa kufanya nini?" Abu Awad aliuliza. Kijana huyo hana matumaini makubwa ya msaada ili kubadili hatima yake. "Hakuna mtu anayetujali."