Urusi yaendeleza mashambulizi kwenye maeneo ya Ukraine
31 Machi 2022Maafisa wa Ukraine wamesema vikosi vya Urusi vimeshambulia viunga vya mji mkuu wa Ukraine, Kiev na mji wa kaskazini wa Chernihiv saa chache baada ya kuahidi kupunguza mashambulizi kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, tangazo hilo la Urusi lilitiliwa mashaka na mataifa ya Magharibi ambayo yalisema hizo zilikuwa njama za Urusi kujipanga upya kwa ajili ya mashambulizi mengine.
Akihutubia Jumatano usiku kwa njia ya video, Zelensky amesema mazungumzo ya amani kati ya nchi yake na Urusi yanaendelea, lakini hakuna matokeo madhubuti yaliyopatikana hadi sasa. Mpatanishi wa Ukraine, David Arakhamia amesema mazungumzo hayo yataendelea Ijumaa tarehe 1 Aprili, baada ya duru ya hivi karibuni kumalizika mjini Istanbul, Uturuki. Arakhamia amesema Jumatano kuwa nchi yake imependekeza viongozi wa nchi hizo mbili wakutane, lakini Urusi imejibu ikisema kazi zaidi inahitaji kufanywa kuhusu rasimu ya mkataba.
Aidha, Urusi imesema imetangaza kusitisha kwa muda mapigano kwenye mji wa Mariupol ili kuruhusu raia kuondoka kwenye eneo hilo. Kamanda wa Urusi, Meja Jenerali Mikhail Mizintsev amesema mapigano yatasitishwa kuanzia Alhamisi saa nne asubuhi kwa saa za Ukraine. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundi yamesema Ukraine ilipewa hadi muda wa saa 12 asubuhi kuthibitisha kuhusu mpango wa kuwaondoa raia kutoka mji huo wa bandari katika Bahari ya Azov kwenda Berdyansk na kisha kuelekea kwenye mji wa Zaporizhzhia.
Marekani kuipatia Ukraine dola milioni 500
Rais wa Marekani, Joe Biden Jumatano usiku alizungumza kwa njia ya simu na Rais Zelensky ambapo wamejadiliana kuhusu uwezekano wa kulisaidia zaidi jeshi la Ukraine. Ikulu ya Marekani imesema kuwa Biden amemwambia Zelensky kwamba Marekani itaipatia serikali ya Ukraine msaada wa moja kwa moja wa dola milioni 500, wakati ambapo nchi hiyo inapambana na uvamizi wa majeshi ya Urusi.
Soma zaidi: Marekani yaahidi msaada mpya wa dola milioni 60 Ukraine
Viongozi hao wawili wamejadiliana kuhusu juhudi za Marekani na washirika wake ambazo zinaendelea kutambua haja ya kulisaidia jeshi la Ukraine kulilinda taifa hilo. Kabla ya tangazo la jana, serikali ya Biden tayari ilikuwa imetoa kiasi cha dola bilioni 2 kwa ajili ya msaada wa kiutu na kiusalama tangu kuanza kwa vita mwezi uliopita.
Huku hayo yakijiri, afisa wa ngazi ya juu wa wizara ya ulinzi ya Marekani amesema vikosi vya Urusi vimeanza kuondoka katika eneo ambako kuna kinu cha nishati ya nyuklia cha Chernobyl, baada ya kuchukua udhibiti kamili Februari 24. Amesema Chernobyl ni eneo ambako wanajeshi hao wameanza kuondoka wakielekea Belarus.
Ujerumani: Putin akubali euro kuendelea kulipia gesi
Wakati huo huo, Ujerumani imesema Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekubali kuendelea kuiuzia Ulaya gesi kwa kutumia sarafu ya euro. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Ujerumani imeeleza kuwa Putin ameitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz. Putin amesema makampuni ya Ulaya yanaweza kuendelea kununua gesi kwa sarafu ya euro. Putin amesema fedha hizo zitalipwa katika Benki ya Gazprom, ambayo haijawekewa vikwazo na kisha zitabadilishwa katika sarafu ya Urusi ya ruble.
Hata hivyo, Sholz hakukubaliana na utaratibu huo, na badala yake amemtaka Putin kumtumia taarifa ya maandishi kwa ufafanuzi zaidi. Wiki iliyopita, Putin alisema nchi ''zisizo rafiki'' zikiwemo za Umoja wa Ulaya zitalazimika kulipia gesi ya Urusi kwa sarafu ya nchi hiyo, ruble. Kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 zimesema malipo ya ruble yatakiuka mikataba iliyopo.
Soma zaidi: Ujerumani yaonya kususia nishati ya Urusi
Mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya Marekani, Kate Bedingfield amesema Rais Putin alipewa taarifa zisizo sahihi na washauri wake ambao waliogopa kumwambia ukweli jinsi vita vya Ukraine vinavyoendelea na jinsi vikwazo vya nchi za Magharibi vinavyoleta madhara makubwa kwa uchumi wa Urusi.
Taarifa kama hizo zimetolewa pia na Uingereza, baada ya mkuu wa idara ya ujasusi Jeremy Fleming kusema kuwa Putin amekuwa akipewa taarifa za uwongo kwa kiasi kikubwa. Fleming amesema wanaamini washauri wa Putin wanaogopa kumwambia ukweli.
Ama kwa upande mwingine Slovakia imewafukuza wafanyakazi 35 wa ubalozi wa Urusi nchini humo kwa tuhuma za uajsusi. Kulingana na taarifa za kijasusi kuhusu shughuli za mwanadiplomasia mwingine wa Urusi ambazo zinakiuka Mkataba wa Vienna kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia, balozi wa Urusi ameitwa kujieleza. Hayo yameelezwa Jumatano usiku na wizara ya mambo ya nje ya Slovakia.
Marekani: Vita vya Ukraine vina ''madhara makubwa'' kwa ulimwengu wa Kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine una athari mbaya kwa ulimwengu wa Kiarabu. Matamshi hayo ameyatoa jana kwenye mji mkuu wa Algeria, Algiers nchi anayoizuru baada ya kutoka Israel ambako alihudhuria mkutano wa kilele kati ya Israel na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tatu za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Morocco ambazo zilifufua uhusiano wao na Israel, 2020 pamoja na Misri ambayo imekuwa na amani na Israel kwa miaka 43.
Akizungumza na waandishi habari, Blinken amesema wakati vita vya Ukraine vinaonekana viko mbali, tayari vina madhara makubwa kwa wananchi wa kanda hiyo. ''Vina madhara ya moja kwa moja kwenye maisha yao kwa sasa, hasa kutokana na kuongezeka kwa bei za chakula na hasa ngano,'' alifafanua Blinken.
Nchi za Afrika Kaskazini zinategemea kwa kiasi kikubwa mauzo ya ngano, na Urusi na Ukraine ndiyo walimaji wakubwa wa ngano.
(AFP, DPA, AP, Reuters, DW)