1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaelezea matumaini ya suluhu katika mvutano na Urusi

9 Februari 2022

Waziri mkuu wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema anaona kupatikana kwa ufanisi katika juhudi za kimataifa za kuzuia uwezekano wa vita na Urusi na kwamba diplomasia inafanya kazi na inazuia dhamira kali za Urusi.

https://p.dw.com/p/46lAY
Dmytro Kuleba | Ukrainischer Außenminister in Dänemark
Picha: Mads Claus Rasmussen/AP Photo/picture alliance

Wakati wanajeshi 100,000 wa Urusi wakiwa bado wamekusanyika karibu na mipaka ya Ukraine, Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema diplomasia inaendelea kupunguza mvutano. Kuleba amewaambia wanahabari kwamba jinsi Umoja wa Ulaya utakavyokabiliana na mgogoro huo, itaamua mustakabali wa usalama wa Ulaya na wa kila taifa la Ulaya.

Kuleba asema vikwazo dhidi ya Urusi bado vitakuwepo

Kuleba amesema Ukraine imekuwa ikiangaziwa zaidi katika siasa za kimataifa katika siku za hivi karibuni kutokana na ziara za viongozi wa mataifa ya Magharibi na serikali na kwamba Urusi sasa inafahamu kuhusu vikwazo dhidi yake iwapo itaishambulia Ukraine. Kuleba ameongeza kuwa vikwazo vilivyotayarishwa bado vitakuwepo hata baada ya kupungua kwa mvutano na vitaendelea kuitishia Urusi.

Waziri huyo ameendelea kusema kuwa zaidi ya tani elfu 1 za risasi na silaha zilizopelekwa nchini Ukraine zimeanza kuwa na athari na kwamba hii sio hali aliyotarajia rais wa Urusi Vladimir Putin .

Siku ya Jumatano, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliendelea kuimarisha juhudi za kuzuia uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine wakati mataifa hayo mawili yakisema yanaona mwangaza katika kutatua mvutano ulioko.

Deutschland | Bundeskanzler Olaf Scholz
Olaf Scholz - Kansela wa UjerumaniPicha: Michele Tantussi/Getty Images Europe/Pool/dpa/picture alliance/

Scholz, aliyekabiliwa na shtuma nchini mwake kutokana na hatua za kutatanisha kuhusiana na mzozo wa Ukraine, anaongeza kasi yake ya kidiplomasia ili kuwahakikishia washirika wake kwamba Ujerumani haitakuwa kiungo dhaifu zaidi miongoni mwa washirika katika hatua dhidi ya Urusi.

Chini ya saa 24 baada ya ziara yake nchini Marekani kusisitiza azimio lake kwa rais wa nchi hiyo Joe Biden hapo Jumanne, Scholz alisimama pamoja na rais wa Poland Andrzej Duda na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza Umoja wa Ulaya katika lengo lao la kuepusha vita katika bara hilo. Kiongozi huyo wa Ujerumani atafanya mazungumzo na waziri mkuu wa Denmark Mette Frederiksen kabla ya kushiriki katika mlo wa jioni na Rais wa baraza la Ulaya Charle Michel baadayeJumatano.

Scholz kufanya ziara Ukraine na Urusi

Wiki ijayo, Scholz atasafiri kulekea Ukraine na kisha Urusi ambapo atakuwa na mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana na Putin ambaye ametaka dhamana nyingi za kiusalama kutoka kwa jumuiya ya kujihami ya NATO na Marekani. Baada ya mazungumzo yake na Macron, Putin alisema kwamba atafanya kila awezalo kuafikia maelewano ambayo yatamfaa kila mmoja.