1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaomba vikwazo zaidi dhidi ya Iran

Saleh Mwanamilongo
17 Oktoba 2022

Ukraine imetaka Iran iwekewe vikwazo zaidi baada ya kusema ndege za Iran zisizo na rubani zimetumiwa na Urusi kushambulia mji mkuu wa Kyiv hii leo.

https://p.dw.com/p/4II7z
Afisa wa polisi akitazama vifusi vya mawe na ardhi vikiruka angani huku ndege zisizo na rubani za Urusi aina ya Kamikaze zikipiga katikati ya mji mkuu wa Kyiv, Ukraine.
Afisa wa polisi akitazama vifusi vya mawe na ardhi vikiruka angani huku ndege zisizo na rubani za Urusi aina ya Kamikaze zikipiga katikati ya mji mkuu wa Kyiv, Ukraine.Picha: Vadym Sarakhan/AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ametoa wito wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran, saa chache baada ya Kyiv kushambuliwa na kundi la ndege zisizo na rubani za Kamikaze, na kusabisha vifo vya takriban watu watatu.

Kwenye mtandao wake wa Twitter, Kuleba aliomba ulinzi zaidi wa anga na usambazaji wa risasi kwa Ukraine. Pia alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Iran kwa kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani ambazo Urusi imekuwa ikitumia nchini Ukraine.

Asubuhi ya leo, Kviv, mji mkuu wa Ukraine, ulikumbwa na wimbi la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za kujitoa mhanga zilizojaa vilipuzi. Ndege hizo zisizo na rubani zilionekana kujumuisha  zile za aina ya ''Shahed'' zilizotengenezwa na Iran.

''Malengo yote yalifikiwa''

Bila kuelezea ikiwa wametumia ndege zisizo na rubani kutoka Iran, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi, Igor  Konashenkov amesema operesheni za kijeshi zilizoendeshwa UKraine hii leo zinafikia malengo yake.

''Katika saa 24 zilizopita, Vikosi vya Wanajeshi vya Shirikisho la Urusi viliendelea kufaya mashambulizi kwa silaha za masafa marefu za anga na baharini dhidi ya vifaa na udhibiti wa kijeshi na mfumo wa nishati wa Ukraine. Malengo yote yalifikiwa." ,alisema  Konashenkov.

Kinu cha nyuklia kimekatwa na mawasiliano ya umeme

Wakaazi wa Kyiv wakikimbia mashambulizi ya ndege zisiso na rubani
Wakaazi wa Kyiv wakikimbia mashambulizi ya ndege zisiso na rubaniPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Wanajeshi wa Ukraine walifyatua risasi hewani wakijaribu kuangusha ndege hizo ndogo zisizo na rubani baada ya milipuko kutikisa katikati mwa Kyiv. Kinga ya mashambulizi ya roketi ilionekana katika anga, ikifuatiwa na mlipuko huku wakazi wakikimbia kutafuta mahali pa kujificha.

Meya wa mji wa Kyiv, Vitali Klitschko alisema mwanamke mjamzito alikuwa miongoni mwa watu watatu waliouawa katika shambulio hilo kwenye jengo la makazi. Kwa upande Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Denys Monastyrskyi alisema kuna vifo katika miji mingine lakini hakutoa idadi kamili.

Wakati huohuo kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kimekatwa mawasiliano kutoka gridi ya taifa ya umeme hii leo kufuatia mashambulizi ya Urusi na kusababisha majenerata ya dizeli kuanza kutumika. Kituo hicho kinadhibitiwa na vikosi vya Urusi.

Kubadilishana wafungwa

Huku hayo yakijiri, Urusi na Ukraine zinatarajiwa kubadilishana hii leo jumla ya wafungwa 220. Denis Pushilin, mkuu wa mkoa wa Donetsk anayeungwa mkono na Moscow amesema Waukraine 110, wengi wao wakiwa wanawake,wataachiliwa kwa zamu ili kuachiliwa kwa Warusi wakiwemo mabaharia wa kiraia 80 na wa wafanyakazi wa kijeshi 30.