Ukraine yasema jeshi lake laendelea kusimama imara
23 Machi 2022Kwa mujibu wa tangazo la kamandi kuu ya jeshi la Ukraine, vikosi vya Urusi vimeshindwa kusonga mbele katika maeneo mengi ya Ukraine, likiwemo la Sloviansk katika mkoa wa Donetsk kusini mashariki mwa nchi hiyo. Tangazo hilo pia limesema kuwa mji wa Mykolaiv umelindwa vizuri upande wa kusini, kama ulivyo ule wa Chernihiv upande wa kaskazini mashariki.
Soma zaidi: Zelensky awataka raia wa Ukraine kuendelea na mapambano
Katika mji wa Mariupol ambao umeshuhudia mojawapo ya mapigano makali zaidi katika vita hivi, kamandi ya jeshi la Ukraine imesema katika tangazo lake kuwa wanajeshi wao wamejizatiti na kujilinda dhidi ya mashambulizi kutoka kila upande.
Watu laki moja bado wamekwama Mariupol
Kwa mujibu wa rais wa Ukraine, watu wapatao 100,000 bado wamenaswa katika mji huo wa bandari uliozingirwa, na kuongeza lakini kuwa wengine makumi kwa maelfu wameweza kuondoka wakiwemo wapatao 7,000 walioukimbia mji huo katika muda wa saa 24 zilizopita.
Kwa upande wake, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema katika taarifa yake kuwa hilikopta ya yao chapa Ka-52 imelishambulia na kuliharibu ghala ya silaha ya Ukraine, bila hata hivyo kueleza mahali ilikofanyika hujuma hiyo.
Soma zaidi: Biden adai Urusi inakusudia kutumia silaha za kemikali
Ukraine inadai kuwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi Februari 24, imeweza kuziangusha na kuziharibu ndege za Urusi zipatazo 100. Madai hayo na taarifa zote zinazotangazwa na pande hizi kuhusu yanayojiri kwenye uwanja wa vita, ukweli wake hauwezi kuthibitishwa.
Mazungumzo 'magumu' yaendelea
Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy amesema mazungumzo baina ya nchi yake na Urusi yanaendelea kila siku, akiyataja kuwa magumu sana, kutokana na masharti magumu ya Urusi ambayo amesema wakati mwingine yanaonekana yanaonekana kuwa yenye nia mbaya.
Urusi kwa upande wake imeilaumu Marekani kwa kukwama kwa mazungumzo baina ya Moscow na Kiev. Waziri wake wa mambo ya nje, Sergei Lavrov amesema wajumbe wa Ukraine katika mazungumzo hayo wanabadilisha msimamo kila wakati, na kuongeza kuwa ''mtu hawezi kujizuia kushuku kuwa wanafungwa mikono na Wamarekani''.
Soma zaidi: Ukraine yakataa wito wa Urusi kwa Mariupol kujisalimisha
Katika ujumbe wake kwa njia ya vidio, kiongozi huyo wa Ukraine amesema anayo matumaini kuwa mikutano mikubwa muhimu itakayofanyika wiki hii, ikiwemo ya kundi la nchi za kidemokrasia zinazoongoza kiviwanda, G7, Jumuiya ya Kujihami ya NATO pamoja na Umoja wa Ulaya, itaongeza msaada kwa Ukraine na kuzidi kuibana Urusi kwa vikwazo.
Vyanzo: dpae, ape